Majonzi Koffi Annan akizikwa
PETER MBURU na AFP
Ulimwengu na raia wa Ghana Alhamisi waliomboleza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Mataifa (UN), Koffi Annan katika hafla ya kusherehekea uhai wake jiji kuu la Accra, Ghana.
Mwili wa Bw Annan ulifika nchini humo kutoka Uswizi Jumatatu ili kusubiri mazishi yatakayofanyika katika kaburi la kijeshi Alhamisi.
Kiongozi huyo wa kidiplomasia aliaga dunia Agosti 18 baada ya kuugua kwa muda mfupi, akiwa na miaka 80.
Jeneza lake likigubikwa bendera ya Ghana na kulindwa na maafisa wakuu wa kijeshi, hafla ya maombolezi iliendelezwa kwa njia shwari katika makao makuu ya Accra.
Bw Fritz Kitcher ambaye alihudumu kama mwanaharakati wa UN Geneva alisema alishuhudia kukua kwa Bw Annan katika ngazi za uongozi.
Alisema Bw Annan alimfunza upole, uaminifu na kuwa na udiplomasia.
Alisema kuteuliwa kwa kiongozi huyo kuwa wa kwanza katika ngazi hiyo UN ilikuwa “heshima kwa Ghana.”
“Ilikuwa kitu ambacho tunaweza kuota tu, aliinua Afrika na kuonyesha kuwa pia nasi tunaweza kuongoza na kufanya mambo makubwa,” akaeleza AFP.
Wengi walimsifu Annan kuwa aliheshimika kote duniani, alikuwa na hekima na busara iliyowafaa wengi.
Viongozi tofauti kutoka Kenya wakiwemo maspika Justin Muturi na Kenneth Lusaka na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamesafiri kwenda Ghana kama baraza litakalomwakilisha Rais Uhuru Kenyatta katika mazishi ya Bw Annan.
Itakumbukwa kuwa ni hayati Annan ambaye alichangia kupatikana kwa Amani nchini Kenya mnamo 2008 wakati vita vilikuwa karibu kumeza taifa baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata Desemba 2007.