Habari Mseto

Dume 'lililosafiri mbinguni' lasema linapanda bangi kwa kuwa ni 'amri ya Maulana'

September 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

POLISI Kaunti ya Kiambu wanamzuilia mwanamume mmoja aliyekamatwa Jumatano kwa kupanda bangi shambani, akidai alifanya hivyo kulingana na amri za Mungu.

Bw Njoroge Mbugua, mkazi wa kijiji cha Nguiru, Limuru alikiri kujihusisha na upanzi wa mmea huo wa dawa haramu ya kulevya kwa miaka miwili.

Alieleza wanahabari kuwa alianza ukulima huo miaka miwili iliyopita baada ya ‘kusafiri hadi mbinguni’, ambapo alipokea ‘amri kutoka kwa Mungu’ kuwa awapandie watumizi wa bangi mmea huo.

“Hii kazi ni yangu peke yangu, hata nikiwacha lakini Mungu ndiye aliniambia nipande sababu nimeenda juu na nikarudi,” akasema mshukiwa.

Aliongeza kuwa amekuwa na wateja wengi kwa kipindi hicho, akisema “watu ni wengi wa kutumia.”

Japo polisi hawakubaini dhamana yam mea huo, waling’oa na kuharibu, huku wakimzuilia mshukiwa, ambaye ametajwa kuwa  anayeishi kivyake na kulinda zao lake vikali.

Kulingana na afisa wa utawala eneo hilo, jamaa huyo huwa amezingira zao laake kwa miti yenye miba huku akitembea na silaha tayari kukabiliana na yeyote atakayetatiza kilimo chake.

“Huwa anabeba panga, rungu silaha zingine, huwezi kumkaribia,” akasema chifu huyo.

Polisi waling’oa mimea iliyonawiri ya zao hilo na kuibeba kwa gari lake baada ya kumkamata mshukiwa akitarajiwa kufikishwa kortini.