Naibu Rais aliyegeuka pasta aponea kifungo akidai wafuasi watahangaika
BBC NA PETER MBURU
ALIYEKUWA Naibu wa Rais nchini Zambia Nevers Mumba aliepuka kifungo jela baada ya kujitetea mahakamani kuwa akifungwa wafuasi wake watateseka na kuhuzunika, kwani alibadilika na kuwa pasta.
Mwanasiasa huyo wa zamani na mhubiri kwa sasa alipatikana na makosa ya matumizi mabaya ya afisi na mamlaka na mahakama moja ya chini Jijini Lusaka Jumanne.
Mashtaka yalihusiana na makosa aliyotenda alipokuwa balozi wa Zambia nchini Canada kati ya 2009 na 2011.
Alipatikana na makosa ya kupeana kandarasi kwa kampuni moja kutoka Canada kufanya kazi za umeme katika makao makuu ya Kamishna Mkuu.
Aidha, Bw Mumba alihukumiwa kwa makosa ya kutofuata mchakato uliofaa wakati wa kupeana kandarasi nyingine ya kazi za umeme na ujenzi katika makao hayo.
Lakini akijitetea baada ya kupatikana na makosa, Bw Mumba alisema kuwa wafuasi wake wa dini hawangetoboa bila yeye, akieleza korti kuwa ikimfunga watateseka.
Hakimu alionekana kumwonea huruma naibu huyo wa Rais wa zamani aliyehudumu kati ya 2003 na 2004, na kumwachilia huru.
Lakini gazeti moja la nchi hiyo ambalo ni la serikali lilisema kuwa kuhukumiwa kwake kulimaanisha kuwa hawezi kugombea Urais tena.
Hii ni licha ya kuwa amekuwa mhusika katika ngazi za kisiasa, akishikilia wadhifa wa kitengo kimoja cha kilichokuwa chama cha uongozi MMD.