Wanaofanya biashara na mashirika yasiyo na PIN ya KRA waonywa
Na BERNARDINE MUTANU
Shirika la Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) limetoa onyo kwa watu na mashirika ambayo yanafanya biashara na kampuni na watu ambao nambari zao za utambulisho katika kulipa ushuru (PIN) haziko katika jukwaa la i-Tax.
Kulingana na KRA, PIN zote ambazo hazimo i-Tax ni batilifu, na wafanyibiashara wanatumia njia hiyo kukwepa kulipa ushuru.
Kulingana na afisa mkuu wa ukusanyaji wa ushuru wa humu nchi Bi Judith Njagi, mashirika hayafai kukubali PIN zozote zizizoko I-Tax.
I-Tax ni mfumo mpya wa kuandikisha ushuru na kupata PIN. KRA inalenga kupanua kiwango cha mahali ambako inapata ushuru baada ya kukosa kutimiza malengo yake ya ushuru katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.
Shirika hilo lilishindwa kutimiza kiwango hicho kwa Sh172.4 bilioni. Lilikuwa limelenga kukusanya Sh1.65 trilioni, lakini badala yake likakusanya Sh1.48 trilioni.