Michezo

Tottenham kunyima Lloris mshahara wa wiki mbili kwa ulevi

September 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Geoffrey Anene

KIPA Hugo Lloris amepigwa faini ya Sh32,990,269, ambayo inatoshana na mshahara wake wa wiki mbili, na klabu yake ya Tottenham Hotspur baada ya kukiri alipeleka gari akiwa mlevi chakari.

Mfaransa huyu, ambaye aliongoza nchi hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Urusi mwezi Julai, alikamatwa na kushtakiwa na polisi mwezi Agosti na kukiri Septemba 12 kwamba alikunywa pombe zaidi ya maradufu ya kiasi kinachokubalika kisheria.

Lloris alipigwa faini ya Sh6,601,539 na mahakama na marufuku miezi 20 kuendesha gari, na sasa gazeti la Evening Standard limeripoti kwamba Spurs itaongeza adhabu yake.

Spurs, ambayo imeajiri Mkenya Victor Wanyama, inatarajiwa kutoza Lloris faini ya juu kabisa ya klabu hiyo ambayo ni Sh32,990,269, sawa na mshahara wake wa majuma mawili, ingawa kocha Mauricio Pochettino awali amepuuzilia mbali uwezekano wa kumpokonya unahodha wa Tottenham.

Mahakama ya Westminster ilielezwa kwamba Lloris alisaidiwa kutoka katika gari lake la aina ya Porsche lenye thamani ya Sh15,172,525 na alikuwa akipepesuka na kugugumiza kwa sababu ya pombe aliposimamishwa na polisi.

Alikuwa amebeba abiria mmoja. Alionekana akiendesha gari vibaya barabarani jijini London na kukaribia kugonga magari yaliyokuwa yameegeshwa na kisha kuvuka taa za trafiki aliposimamishwa na polisi.

Lloris amekosa mechi tatu zilizopita, ingawa kwa sababu ya jeraha la misuli ya paja wala si kutokana na kuendesha gari vibaya.