Kwaheri Volkswagen Beatle
MASHIRIKA Na PETER MBURU
KAMPUNI ya kutengeneza magari ya Volkswagen imetangaza kukomesha utengenezaji wa gari la kihistoria aina ya ‘Beatle’ kuanzia 2019.
Kampuni hiyo imeamua kumaliza gari hilo ambalo lilipata umaarufu ulimwenguni miaka ya zamani, wakati ikichangamkia utengenezaji wa magari ya kielektroniki.
Kampuni hiyo ilisema sasa inaangazia kutengeneza magari ya kifamilia, ambayo yatabeba watu wengi kwa pamoja. Maafisa wake walidokeza uwezekano wa kutimiza ahadi waliyoweka 2017, kuja na basi jipya la kisasa.
“Tunapoelekea kutengeneza magari ya aina zote, magari ya kufaa familia huku US na kumalizia mradi wa kutengeneza magari ya kutumia nguvu za umeme ndipo tunaelekea,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Volkswagen Hinrich Woebcken.
Lakini kampuni ilikiri kuwa kumaliza gari hilo la Beatle ambalo limekuwa sokoni kwa takriban miaka 70 kunatarajiwa kuibua hisia kutoka kwa mashabiki wake kote duniani.
Magari mawili ya Beatle yanayoundwa yakiwa ya mwisho sasa ni aina za Coupe na Convertible ambayo yatauzwa kuanzia Sh2, 304, 500 kwenda juu, kampuni hiyo ikasema.
Historia ya gari hilo inatokana na enzi za Nazi, Ujerumani na ilitengenezwa na Ferdinand Porsche akisaidiwa na Dikteta Adolf Hitler ambaye mnamo 1937 aliunda kampuni ya serikali ya Volkswagenwerk baada ya vita vya kwanza vya dunia
Mauzo ya gari hilo katika soko la Marekani mwaka uliopita yalipungua hadi 15,667, asilimia 3.2 pekee.