Wabunge wakaidi pendekezo la Uhuru
BENSON MATHEKA na SAMUEL KAZUNGU
WABUNGE wa upande wa Serikali na upinzani wameonekana kuungana katika kukaidi mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu marekebisho ya Mswada wa Fedha 2018.
Tangu Ijumaa Rais Kenyatta aliporejesha Mswada wa Fedha wa 2018 kwa Bunge na kupendekeza mabadiliko kadhaa ili kusaidia kupunguza kiwango cha VAT ya mafuta kutoka asilimia 16 hadi 8, wabunge wa NASA na Jubilee wamekuwa wakiapa kukataa mapendekezo hayo.
Hasira ya wabunge ni kuwa rais alipunguza bajeti ya Bunge na Hazina ya Maeneobunge (CDF), lakini hakugusa ya serikali kuu. Bajeti zilizopunguzwa ni pesa zilizotengewa miradi ya maendeleo katika serikali za kaunti kwa Sh9 bilioni, pesa zilizotengewa usawazishaji wa kaunti kwa Sh3.8 bilioni, bajeti ya bunge kwa Sh9 bilioni na hazina ya Maeneobunge kwa Sh5 bilioni.
Pia Rais Kenyatta alipendekeza kupunguzwa kwa bajeti ya usafiri na shughuli zingine zisizo muhimu, hatua ambayo itakuwa na athari kwa wabunge.
“Mbunge yeyote anayefahamu kazi yake, anafaa kukataa jaribio la Rais la kutumia mlango wa nyuma kutunga sheria. Hatuwezi kuruhusu Wakenya kuteseka. Hatua ya Rais Kenyatta inafaa kukataliwa,” alisema Mbunge wa Saboti Caleb Amisi.
Kulingana na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo (ODM) wakati umefika wa wabunge kuungana kukataa mapendekezo ya Rais Kenyatta.
Wabunge wameitwa kutoka mapumzikoni hapo kesho kujadili mapendekezo ya Rais ambaye alikataa kutia sahihi mswada ambao walikuwa wamependekeza kuahirishwa kwa utekelezaji wa VAT ya mafuta hadi 2020.
Rais alikataa msimamo wa wabunge akisema ni lazima Wakenya walipe ushuru kufadhili miradi ya serikali na akatoa mapendekezo mapya akipunguza ushuru huo hadi asilimia 8.
Lakini dalili zinaonyesha kuwa huenda mvutano ukaendelea hasa kufuatia hatua ya rais ya kupunguza pesa zilizotengewa Bunge na CDF.
Wabunge wanasisitiza kuwa ni lazima ushuru huo uahirishwe kabisa badala ya kupunguzwa.
Duru zinaeleza kampeni dhidi ya mapendekezo ya Rais zilianza Ijumaa.
Tayari wabunge kadhaa wa upinzani wameapa kukataa mapendekezo ya Rais wakisema hayawapi Wakenya afueni yoyote.
Japo kuna juhudi za Jubilee kuwarai wabunge wa upande wa serikali kukubali mapendekezo ya rais, wabunge wamenukuliwa wakiapa kutobadili nia kuhusu ushuru huo.
Mbunge wa Soy, Caleb Kositany (Jubilee) ameahidi kupinga mapendekezo hayo akisema serikali inafaa kupunguza bajeti ya Ajenda Nne Kuu za serikali.
Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Murang’a Sabina Chege (Jubilee) kwa upande wake amesema hatua zilizochukuliwa na Rais sio nzuri kwa Wakenya. Bi Chege alisema serikali inapasa kupunguza ubadhirifu na kupigana na ufisadi.
Wakifanikiwa kupata wabunge 232 kukataa mapendekezo hayo, mswada huo utakuwa sheria moja kwa moja na hivyo kuahirisha utekelezaji wa ushuru huo hadi 2020.
Hilo likifanyika, Serikali Kuu itakuwa na mtihani mkubwa ikizingatiwa ushuru huo ulikuwa ni masharti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF). Hii inaweza kusababisha kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya, kuwekewa masharti magumu zaidi na IMF na ukuaji wa uchumi kuyumba.
Wakati huo huo, wabunge wa upande wa upinzani watakutana kesho kuamua hatua watakayochukua kuhusu mswada uliokataliwa na Rais Kenyatta.
Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa, Bw John Mbadi, alisema mkutano wao utafanywa kabla mswada huo kuwasilishwa bungeni Jumanne alasiri.
“Kama sababu zilizotolewa na serikali zina msingi, tutazikubali lakini kinyume na hicho, tutachukua hatua ambayo itakuwa kinyume na msimamo wa rais,” akasema Bw Mbadi akiwa Mombasa.
Aliongeza kuwa haijaeleweka wazi mapendekezo ambayo Rais alitoa lakini akaonya kuwa pendekezo la kuleta bajeti ya ziada halifai wakati huu.
“Nikiwa kiongozi wa wachache, nina jukumu la kutoa mwelekeo kwa wanachama wetu punde tutakapoamua kuhusu msimamo tutakaochukua ndiposa tumeitisha mkutano,” akasema Bw Mbadi.