Boti lililoundwa kwa takataka za plastiki lazinduliwa Lamu
NA KALUME KAZUNGU
KAUNTI ya Lamu imeingia kwenye historia kwa kuzindua boti lililotengenezwa kwa kutumia takataka za plastiki zilizookotwa katika ufuo wa Bahari Hindi eneo hilo.
Ulimwenguni kote kuna maboti mawili pekee ambayo yanafahamika kuundwa kwa kutumia takataka za plastiki, moja likiwa Uingereza.
Shughuli ya uzinduzi wa boti hilo ilifanyika katika kisiwa cha Lamu Jumamosi na kuongozwa na Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala.
Boti hilo liliundwa kwa kutumia zaidi ya tani kumi za plastiki zilizozolewa kutoka baharini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mashua hiyo, Bw Balala aliwasifu walioshirikiana kulitengeza, akisema hatua hiyo imesaidia kuweka mazingira safi kwenye ufuo wa bahari.
Alisema hatua ya kutengenezwa kwa boti hilo pia imechangia pakubwa kuhamasisha marufuku iliyopo nchini dhidi ya utumizi wa mifuko ya plastiki.
Marufuku hiyo iliamriwa kote nchini mnamo Agosti 28 mwaka jana, lengo kuu likiwa kuhifadhi mazingira.
“Tunafurahia kwamba leo tuko na boti ambalo limeundwa kwa kutumia mifuko ya plastiki iliyozolewa kwenye fuo zetu. Hii ni hatua ya kuigwa kwani inasaidia kuweka mazingira safi kwenye fuo zetu,”alisema.
Aliongeza, “Tujiepushe na matumizi ya plastiki na utupaji wa taka kwenye bahari zetu ili kuepuka maafa ya viumbe baharini.”
Aliyebuni mbinu hiyo, Bw Ali Skanda, alisema wamechukua muda wa miaka miwili kuunda boti hilo.
Pia alisema azma yao ni kuhakikisha fuo za bahari eneo la Lamu na Kenya kwa jumla haziathiriwi na uchafu, pamoja na kuhimiza wakazi kukoma kutumia plastiki na kisha kuzitupa baharini.