KURUNZI YA PWANI: Wanawake wajipa ujasiri kupinga ukeketaji
NA STEPHEN ODUOR
IMEPITA miaka 22 tangu Bi Nastehe Aftin kukeketwa kilazima. Alikuwa na umri wa miaka mitano pekee wakati wazazi wake walipompeleka kukeketwa, bila kujali kuwa alichukia mila hiyo iliyowanyanganya hadhi wanawake katika jamii za wafugaji Kaunti ya Tana River.
“Sikutaka kukeketwa lakini wazazi wangu na wakongwe waliokuwa wakiwakeketa wasichana katika jamii hawangetaka kusikia usemi wangu, kwani haukuwa na msingi kwao,”alisimulia.
Asubuhi hiyo ya November 1996, mamake alimwamsha na kumpeleka kwenye foleni walipokuwa wenzake, tayari kwenda unyagoni.
Walichukuliwa na kutengwa na na wenzao, kisha kuekwa ndani ya kijumba kidogo tayari kwa siku ya kuadhimishwa kutoka kwa usichana na kuwa mwanamke.
Kijumba hicho kilikuwa chini ya ulinzi mkali ili kuzuia wakeketwa watarajiwa wasitoroke.
“Tulikuwa chini ya ulinzi mkali na kupewa mafundisho kuhusu umuhimu wa kukeketwa, na yale yaliyotarajiwa kutoka kwetu baada ya kukeketwa,” alieleza.
Mafunzo yalichukua siku nzima, huku wakitiwa motisha na ujasiri kwa kukabiliana na kijembe ambacho wangepitia makali yake asubuhi iliyofuatia.
Siku iliyofuatia waliamshwa mmoja baada ya mwingine, nyimbo za ushujaa na sifa zikiwa zimetanda anga wakielekezwa katika kijumba kingine mwituni, mbali na kijiji ambapo wangelikeketwa.
Ndani ya kile kijumba, wanawake wanane walisimama wima, saba kati yao kazi yao ikiwa ni kuwashika wasichana waliokuwa wakikeketwa ili wasizue rabsha, huku mwanamke mmoja mkongwe akiwa ndiye mtaalamu wa ukeketaji.
Ilipofika zamu yake Bi Aftin, alijipata kashikwa mkekani na wanawake saba, nguo zake zikararuliwa na kutupwa mbali kabaki uchi wa mnyama, miguu yake ikashikiliwa pande mbili, akatanuliwa bila utu.
Alimwagiwa maji baridi kama barafu katika sehemu za siri, ili zife ganzi, mara ghafla kijembe kikapita kwa mara ya kwanza, mara ya pili hangeweza kustahimili, akatoa kamsa ya kuwaamsha wafu mapumzikoni.
“Maji yale hayakusaidia chochote, kijembe kile kilipopita katika sehemu zangu nyeti kilikata bila huruma, walinichana karibia kila kitu cha kunifanya mwanamke katika sehemu hizo na kwa hakika ulikuwa uchungu usiokuwa na kifani,” alisimulia.
Baada ya kukeketwa, wakongwe hao walishona sehemu walizokata kwa uzi, na kisha akafungwa miguu kwa pamoja kutoka kiunoni hadi utosini.
Hakuweza kutembea, na hata kwenda haja ndogo ilikuwa taabu. Ilibidi alale kiupande ili kufanikisha haja hiyo, na mara nyingi aliyafanya pale alikoketi.
Mkeketaji aliwatembelea mara kwa mara akichungunguza kazi yake na kuwapa matibabu, ole wao vidonda vyao vilivoonyesha dalili za kuongezeka kutokana na maambukizi.
“Kwa wale ambao vidonda vya vilionyesha dalili za kuathirika, mkeketaji alivifungua na kisha kutumia chuma moto kuchoma sehemu ile ili kuuwa maambukizi yoyote,” alieleza.
Walikaa mafichoni kwa miezi sita, na iliposhukiwa kuwa sasa wamepona, kina mama wale wakongwe walikuja wakiwa wamendamana na karibia kijiji kizima, shangwe na vifijo vikitanda angani.
Huku wengine wakifurahia uhuru wao, wakitembea kwa madaha na kucheza goma za kitamaduni ya Wardei, Bi Aftin alikuwa na huzuni tele.
Punde alipopata fursa ya kuwa huru, mguu wake wa kulia haungeweza kusonga sawia na ule wa kulia, ulikuwa umepooza kwa kufungwa na kukosa mtiririko kamili wa damu.
“Wazazi wangu walinibeba mpaka nyumbani na baada ya muda nikaanza kutembea na kigogo. Singeweza kusherehekea kama wenzangu. Hapakuwa na sherehe kwetu, ukeketaji ulizalisha mlemavu kwetu,” alieleza kwa huzuni.
Bi Aftin sasa amejifunza kuchechemaa katika wimbi la furaha, kujikubali na kutumia hali yake kama kielelezo kwa wazazi na wasichana wengine kupinga ukeketaji wa jinsia ya kike.
Amekuwa mwanamziki wa kutajika na kutunga nyimbo kumi kupinga ukeketaji, na pia ni mwanzilishi wa kundi la wanaharakati wa kupinga ukeketaji la Dayaa, katika Kaunti ya Tana River.
Sio yeye tu aliye na hadithi za huzuni. Bi Amina Salima Ware kutoka jamii ya Waorma alieleza jinsi madhara ya ukeketaji yalianza kubainika pale alipoolewa.
Bi Ware alipoteza mimba nne mfululizo kwani sehemu ya kujifungua ilijuwa ndogo sana kutokana na jinsi alivyokuwa kashonwa baada ya kukeketwa.
Hapakuwa na usaidizi wa wataalamu halisi, kwani alikuwa mbali na hospitali ya mji. Pia jamii iliwaamini wakongwe wa kijiji kufanikisha mambo kama yale, ila kila mara walifeli.
“Kule nyumbani hata walionikeketa walishindwa jinsi ya kunisaidia, na kila mara mtoto angetoka kama amekufa,” alisimulia kwa uchungu.
Uhusiano kati yake na mume wake pia haukuwa wa kufana, kwani nafasi iliyokuwa imeachwa baada ya ukeketaji ilikuwa ndogo mno, ya kupitisha haja ndogo tu.
Baadaye alipewa talaka akaenda kuishi kwa dadake mjini Hola. Kwa mshangao wake, alikuwa mja mzito wa mwezi mmoja alipopewa talaka.
Akiwa kwa dadake aliilea mimba ile kwa umakini mkubwa, huku akipokea ushauri wa madakitari wa hospitali ya Hola, dadake akiwa nguzo kubwa kwake na hatimaye akafanikiwa kujifungua mtoto wa kike.
“Huyu mtoto alinifuta machozi na kuniondolea aibu, alinipa haki kama mama na ni jukumu langu sasa kumtunza na kuhakikisha hapitii niliyopitia, na yeyote atakayejaribu kumkeketa hata baada ya kifo changu nimemlaani afe kifo kibaya zaidi,” alisema kwa sauti thabiti na chozi usoni.
Kuna wanawake zaidi ya elfu katika jamii za wafugaji katika kaunti ya Tana River wanaoishi na makovu ya ukeketaji.
Wengine wao wameaga kupitia kijembe hicho hatari,wengine wakifanywa tasa, huku wengine wakiwa wanaishi na maambukizi ya fistula na kwa msanjaa huo huo ni wanaharakati wa kupinga ukeketaji.
Wakiwa katika kikosi kimoja kupinga vita mila na desturi ambazo wamekulia, jamii imewasuta, wazee kuwakemea na hata watoto kukanywa dhidi ya mfano wao huku jamii ikikisia kuwa sio mila na desturi tu, bali dini pia.
Walimu wa dini wamepinga dhana hiyo, wakaungana na wanaharaki wa Dayaa kutoa mafunzo, lakini bado chumvi ya elimu hiyo haijakolea ipasavyo katika jamii.
Watasema leo, kesho, na hata kutwa, lakini msimu wa Disemba unapovizia vizia, wazazi watawaficha wanao na kuvuka nao mipaka ya Garissa kuwakeketa kwa kuhofia kutiwa nguvuni.
Wahenga walisema kuwa subira huvuta heri, na kwa wanaharakati na viongozi wa kaunti hiyo, hawajachoka kukemea na kupinga mila hiyo, wakiwa na imani kuwa ipo siku heri itakuja.