Dada ya mkewe Mugabe anaswa kwa kuuza ardhi ya serikali
Na Mashirika
Dada ya Grace Mugabe mke wa aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, alikamatwa kwa madai ya kuuza ardhi aliyopatiwa na serikali na kujipatia faida kubwa miaka minne iliyopita.
Gazeti la serikali la The Herald liliripoti kuwa Shuvai Gumbochuma, alifikishwa katika mahakama ya hakimu jijini Harare Ijumaa.
Inadaiwa kwamba mnamo 2014, Gumbochuma alipatiwa ardhi ya serikali jijini Harare kustawisha kwa kujenga nyumba za bei nafuu lakini badala ya kufanya hivyo aliuza ardhi hiyo na kupata mamilioni ya pesa.
Gumbochuma anakabiliwa na mashtaka mengine mawili ya kupokea ardhi kustawisha miaka miwili iliyopita akitumia kampuni ambayo haikuwa imesajiliwa.
Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5000. Kesi yake ni ya pili ya watu wenye majina makubwa walioshtakiwa wiki jana. Mnamo Alhamisi, aliyekuwa waziri wa afya David Parirenyatwa alikamatwa kwa madai ya kutumia vibaya mamlaka yake kwa kuagiza mabadiliko katika bodi ya kampuni ya dawa Natpharm ambayo yalihujumu kampuni hiyo.
Waziri huyo alikuwa wa kwanza kukamatwa na kitengo maalumu cha kukabiliana na ufisadi kilichobuniwa na Rais Emmmerson Mnangagwa.