Habari Mseto

Ajitumbukiza ziwani na kufa akiogopa polisi

September 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Richard Maosi

Mvuvi asiyekuwa na kibali cha kuvua anahofiwa kufa maji alipozama katika ziwa Naivasha alipofumaniwa na polisi akivua samaki ziwani humo.

Bw David Kilo mhudumu wa mashua ziwani humo, alieleza kwamba mhusika aliyekuwa na wenzake alijirusha majini polisi wanaoshika doria ziwani walipojitokeza.

Kundi la wavuvi limekuwa likivunja sheria kwa kuvua samaki usiku, hivyo basi wavuvi kujaribu kukwepa kukamatwa na polisi.

“Mwenzetu aliyezama alikuwa katika harakati za kutoroka lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa alipozama,” Bw Kilo alisema.

Wapiga mbizi majini walishindwa kupata mwili wake siku ya Jumamosi ziwani walipokita kutwa, wakihofia mawimbi makali yalikuwa yamemsomba.

Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Naivasha alisema bado hajapokea taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.

“Nitatoa habari kamili baada ya kukusanya habari za kutosha na za kuaminika kutoka kwenye eneo la mkasa ,”alisema.

Bw Kilo aliwaonya wavuvi dhidi ya kushiriki uvuvi wakati ambao wamekatazwa. Vilevile wasijihusishe na mambo yanayoweza kuhatarisha maisha yao.

Aliwaomba vijana wanaotegemea uvuvi kama njia ya kujipatia riziki wafuate sheria na kupata stakabadhi muhimu za kuwaruhusu kushiriki uvuvi.