Huenda rekodi ya Kipchoge isivunjwe hivi karibuni
NA GEOFFREY ANENE
WAKENYA Eliud Kipchoge na Gladys Cherono walifanya maajabu kwa kuibuka mabingwa wa mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani jana, huku Kipchoge akipata ufanisi kwa rekodi mpya ya dunia ya saa 2:01:39 ambayo huenda isivunjwe hivi karibuni.
Bingwa wa Olimpiki Kipchoge alifuta dakika moja na sekunde 18 kutoka kwa rekodi iliokuwepo ya saa 2:02:57 ambayo Mkenya mwenzake Dennis Kimetto aliweka akishinda Berlin Marathon mwaka 2014.
Ilikuwa jaribio la tatu la Kipchoge kuvunja rekodi baada ya kuikosa kwa sekunde nane katika London Marathon nchini Uingereza mwaka 2016 na sekunde 35 jijini Berlin mwaka 2017.
Wakenya kutoka matabaka mbalimbali wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Bwana Raila Odinga pamoja wapenzi wa riadha, wamewasifu washindi hawa wapya, ambao walifanya wimbo wa taifa wa Kenya kuimbwa mara mbili jijini Berlin, Jumapili.
Kipchoge, ambaye pia alitawala Berlin Marathon mwaka 2015, ni Mkenya wa tano kuvunja rekodi ya marathon ya wanaume baada ya Paul Tergat (2003, saa 2:04:55), Patrick Makau (2011, saa 2:03:38), Wilson Kipsang’ (2013, saa 2:03:23) na Kimetto (2014, saa 2:02:57). Rekodi hizi zote zilipatikana jijini Berlin.
Vita vya kuwania taji la makala ya 45 ya Berlin Marathon vilitarajiwa kuwa vikali hasa kati ya Kipchoge na Kipsang’, lakini viliishia kuwa mbio ya farasi mmoja.
Kipchoge aliongoza mbio hizi za kilomita 42 zilizovutia washiriki 40, 000 kutoka mwanzo hadi utepeni.
Mkimbiaji huyu, ambaye amefananishwa na nyota wa zamani wa mbio fupi Mjamaica Usain Bolt kutokana na kwamba ameshinda marathon 10 kati ya 11 ameshiriki na tisa zilizopita, alionyesha dalili za kuvizia rekodi ya Kimetto mapema.
Alikamilisha kilomita ya kwanza kwa dakika mbili na sekunde 43 akifungua mwanya wa karibu mita 25 kati yake na kundi la pili la Kipsang’, ishara kwamba kasi yake ilikuwa juu kuliko alivyopanga.
Mkimbiaji huyu, ambaye rekodi hii ni zawadi ya mapema ya kusherehekea siku kugonga miaka 34 hapo Novemba 5, hakulegeza kamba. Alikamilisha kilomita ya tano kwa dakika 14:24, kilomita 10 kwa dakika 29:01 kabla ya mwekaji wake wa kwanza wa kasi kuondoka baada ya kilomita ya 15, ambayo Kipchoge alikamilisha kwa dakika 43:57.
Wakati huo kasi yake ilikuwa imepungua kidogo, ingawa wawekaji wake wawili waliokuwa wamesalia walihakikisha kasi inaongezeka. Alipita alama ya kilomita 20 kwa dakika 57:56, huku Kipsang’ na Amos Kipruto wakimfuata dakika moja nyuma. Alisalia na mwekaji kasi mmoja Josphat Boit hadi kilomita ya 25, ambayo alikamilisha kwa saa 1:12:24.
Aliongeza kasi na kumaliza kilomita 30 kwa saa 1:26:45. Kasi ya Kipchoge iliongezeka kati ya kilomita 32 na 34 akakamilisha sehemu hiyo kwa dakika 2:49 na alipokamilisha kilomita ya 40 kwa saa 1:41:01, ilionekana wazi akakata utepe chini ya saa 2:02. Wakenya Amos Kipruto (2:06:23) na Kipsang (2:06:48) walimaliza katika nafasi za pili na tatu, mtawalia.
Cherono alinyakua taji lake la tatu jijini Berlin baada ya mwaka 2015 na 2017 kwa kutimka kwa saa 2:18:10, ambayo ni rekodi mpya ya Berlin Marathon.
Mkenya huyu alichukua uongozi kutoka kwa Muethiopia Tirunesh Dibaba katika kilomita ya 25. Dibaba alimaliza katika nafasi ya tatu kwa saa 2:18:55 nyuma ya Muethiopia mwenzake Ruti Aga (2:18:34). Bingwa wa dunia Edna Kiplagat kutoka Kenya alifunga nne-bora kwa saa 2:21:18.
Kampuni ya magari ya Isuzu Kenya, ambayo ilimuahidi gari la Sh20 milioni akifuta rekodi ya Kimetto ilikuwa moja ya watu waliopongeza Kipchoge kwa ufanisi wake. “Tumepata mshikilizi mpya wa rekodi ya dunia!!! Hongera kwa balozi wetu wa magari ya aina ya Isuzu Dmax, Eliud Kipchoge!!! 2:01:38!!!”
Kipchoge na Cherono walizawadiwa Sh4.6 milioni kila mmoja kwa ushindi wao. Kipchoge aliongezwa bonasi ya kuvunja rekodi ya dunia kutoka waandalizi ya Sh6.9 milioni. Cherono pia alijishindia bonasi ya karibu 5.5 milioni kwa kuweka rekodi mpya ya Berlin Marathon baada ya kufuta ile ya saa 2:19:12 Mjapani Mizuki Noguchi alitimka mwaka 2005.
Kuna bonasi ya kuvunja rekodi ya dunia pia kutoka Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF). Vilevile, Kipchoge anatarajiwa kuvuna vinono kutoka kwa kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike, ambayo inamdhamini kutumia bidhaa zake.