Wanaopigania bangi ihalalalishwe wanasaka umaarufu – Mututho
Na JOSEPH WANGUI
ALIYEKUWA mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Mihadarati (NACADA) John Mututho, amepinga vikali mipango ya kuhalalisha ukuzaji na matumizi ya bangi nchini.
Bw Mututho alisema kuwa huenda hatua hiyo ikawapoteza vijana, kwa kuwafungulia njia za matumizi ya mihadarati bila kutathmini athari zinazohusishwa nayo.
Pendekezo hilo limetolewa na mbunge wa Kibra Ken Okoth, ambaye tayari amemwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akimwomba kufadhiliwa kutayarisha Mswada wa Kuhalalisha Matumizi ya Bangi.
“Hiyo ni bidhaa hatari sana. Nimeshangazwa na mbunge huyo. Naona hiyo kama njia ya kujitafutia umaarufu kwa kushinikiza kuhalalishwa kwake. Ni njama kama iliyotumiwa kuhalalisha baadhi ya vileo hatari,” akasema Bw Mututho, alipowahutubia wanahabari mjini Nyeri.
Badala yake, aliwaomba wabunge kutounga mkono mswada huo utakapowasilishwa bungeni, kwa msingi kwamba mbunge huyo anawapotosha vijana.
Alishangaa sababu ya Bw Okoth kushinikiza uhalalishaji wa mmea ambao anajua wazi kwamba huharibu utendakazi wa ubongo mwa mwanadamu.
“Hakuna kwa namna yoyote ambapo mtu anayejali maisha ya binadamu anaweza kuunga mkono mswada huo. Wabunge wanapaswa kufahamu kuwa wana wajibu mkubwa wa kulinda watoto wetu,” akasema Bw Mututho, ambaye kwa sasa anahudumu kama mshauri maalum kuhusu masuala ya mihadarati katika serikali ya Kaunti ya Kiambu. Vile vile, anaisidia katika utekelezaji wa Sheria ya Kudhibiti Vileo ya 2018.
Bw Okoth anashinikiza kuhalalishwa kwa mmea huo, kwa msingi kuwa baadhi ya matumizi yake ni muhimu kwa afya ya mwanadamu.
Baadhi ya nchi duniani kama Afrika Kusini zimehalalisha matumizi yake, japo kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa.