Habari Mseto

Waliomuua jamaa yao mchawi waondolewa hukumu ya kifo

September 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Philip Muyanga

WANAUME wanane waliohukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumuua jamaa yao kwa madai ya kuwa mchawi, walipata afueni baada ya mahakama ya rufaa kubadilisha hukumu hiyo kuwa kifungo cha miaka ishirini.

Hata hivyo majaji wa mahakama ya rufaa walikubali uamuzi wa Mahakama Kuu uliowapata na hatia Mtawali Ngawa, Safari Ngawa, Charo Kitsao, Foleni Ngawa, Said Ngawa, Banaka Chome, Ngala Ponda na Abeid Ngawa ya kumuua Bw Kahindi Ngawa Katana.

Majaji wa Mahakama ya Rufaa Wanjiru Karanja, Martha Koome na Daniel Musinga walisema kuwa wakati wanane hao wakihukumiwa kifo, sheria ilikuwa inasema kuwa hukumu ya kifo ni lazima, lakini Mahakama ya Juu baadaye ilisema hukumu ya kifo ni kinyume cha Katiba.

Waliongeza kusema kuwa wamezingatia ushahidi uliotolewa upya na kwamba walikuwa wanakubaliana na mahakama kuu ya kuwa ushahidi ulikuwa unaambatana na kwamba wanane hao walikuwa katika eneo la tukio.

Katika rufaa yao, wahukumiwa hao walisema kuwa ushahidi dhidi yao ulikuwa ni wa kutungwa, chanzo cha kifo hakikuwa kimejulikana, utetezi wao haukutiliwa maanani na kwamba hukumu yao haikuwa sawa.

Upande wa mashtaka kupitia Bw Vincent Monda ulikuwa umepinga rufaa hiyo ya wanane hao. Wanane hao walimuua Bw Katana mnamo Julai 21 2012 katika kijiji cha Matano Manne kaunti ya Kilifi.