TAHARIRI: Maneno hayatasaidia Kenya kupata ustawi
NA MHARIRI
AZMA ya Rais Uhuru Kenyatta kuacha kumbukumbu kupitia Ajenda Nne Kuu itabakia kuwa ndoto kutokana na jinsi utekelezaji wake unavyoendeshwa.
Hii ni kwa sababu hatua zinazochukuliwa na Serikali zinavuruga badala ya kufanikisha ustawi. Maneno ndiyo mengi kuliko hatua zinazoweza kutekelezeka ili kuwafaa Wakenya.
Kwa mfano yale yanayotendeka katika kilimo yataua sekta hii muhimu badala ya kuiinua. Mfano mzuri ni kuongezwa kwa VAT kwenye dawa za kuua wadudu. Inawezekana vipi useme unataka kusaidia wakulima kuzalisha chakula zaidi na huku unawaongezea gharama za kuzalisha chakula hicho?
Pia Serikali haiwezi kutoa hakikisho kwa wakulima hasa wa mahindi kuwa itawasaidia kupata soko la mazao yao ikizingatiwa yaliyotendeka majuzi ambapo badala ya kuwasaidia wakulima kuuza mazao yao, walaghai ndani ya Serikali walishirikiana na wafanyabiashara kununua mahindi kutoka nje ya nchi. Hili limewavunja moyo wakulima wengi, hali ambayo haichangii katika kuinua kilimo.
Serikali pia inaendelea kutazama kilimo cha kahawa kikiendelea kuangamia kutokana na usimamizi mbaya, wakulima kunyanyaswa na kodi za kila aina ambazo matokeo yake ni kuwaweka wakulima wa kahawa katika umaskini wa kusikitisha.
Hali hii ya Serikali kukosa umakinifu katika mipango yake hasa malengo manne yataacha nchi hii katika hali mbaya kuliko ilivyokukuwa 2013.
Katika utawala wake, Mzee Kibaki alikuwa na maono makubwa ya kuendeleza Kenya kufikia upeo wa juu kimaendeleo na kuwakomboa wananchi kutokana na umaskini.
Alipokabidhi uongozi kwa Jubilee, kwenye hotuba yake Mzee Kibaki aliambia viongozi wa Jubilee kuwa amewaachia taifa lililokuwa tayari kupaa. Lakini sasa inasikitisha kuwa badala ya kupaa ndege ya Kenya inaenda kinyumenyume na hakuna dalili kuwa itapaa karibuni.
Marubani walioachiwa ndege hii wanaonekana kushindwa jinsi ya kufanikisha hilo, na badala yake wanatafuta mbinu zenye maneno makubwa makubwa, lakini inapofika kutekeleza wanafanya kinyume na wakiendelea hivi ndege ya Kenya itasimama kabisa.
Huu ni wakati mwafaka kwa Rais Uhuru Kenyatta kuangazia upya jinsi Serikali yake inavyoendeshwa na aliopatia majukumu mbalimbali, na atagundua kuwa wengi wao ni maadui wa taifa hili.