HabariSiasa

OBADO BADO MAHABUSU

September 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Migori Okoth Obado ataendelea kuwa mahabusu kwa siku mbili zaidi katika gereza la Industrial Area jijini Nairobi, akisubiri iwapo mahakama itamwachilia huru kwa dhamana hapo Alhamisi.

Kuendelea kuwa kizuizini kwa gavana huyo kunafikisha siku sita kufikia leo, ambazo amekuwa mgeni wa Serikali – siku tatu katika kituo cha polisi cha Gigiri na zingine katika gereza la Industrial Area. Hii ni baada yake kukamatwa Ijumaa wiki iliyopita na kisha kushtakiwa mnamo Jumatatu kwa mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.

Alikanusha shtaka la kumuua Sharon usiku wa Septemba 3, 2018 katika eneo la Owade, kaunti ndogo ya Rachuonyo, Homa Bay.

Jana, Jaji Jessie Lessit wa Mahakama ya Milimani aliagiza Bw Obado aendelee kuzuiliwa hadi kesho saa nane atakapoamua ikiwa atamwachilia huru kwa dhamana.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kupitia kwa viongozi wa mashtaka alifichua mahakamani kuwa atamfungulia Bw Obado shtaka jipya la kumuua mtoto ambaye alikuwa tumboni mwa Sharon.

Naibu DPP, Bw Alexander Muteti alisema ni jukumu la Serikali kulinda maisha ya kila mmoja ikiwa ni pamoja na vijusi.

Uchunguzi wa DNA uliofanywa wakati wa uchunguzi wa kesi hiyo ulithibitisha mtoto huyo alikuwa wa Gavana Obado.

Kiongozi huyo wa mashtaka anayesaidiwa na Jacob Ondari na Tom Imbali aliomba mahakama isimwachilie kwa dhamana Gavana Obado akisema wanahofia atavuruga mashahidi na kuwatisha wasifike mahakamani kutoa ushahidi dhidi yake, kwa vile anajua adhabu ya kifo inamkondolea macho.

Jaji alielezwa kuwa Bw Obado yuko na ushawishi mkubwa katika Kaunti ya Migori na itakuwa vigumu kwa mashahidi kujitolea kufika mahakamani kutoa ushahidi dhidi yake iwapo atakuwa huru.

“Tuko na ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi Bw Obado alivyohusika katika kupanga mauaji ya mwanafunzi huyo,” alisema Bw Muteti.

Bw Ondari aliambia mahakama kuwa kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa gavana huyo alihusika katika mauaji hayo akiongeza kuwa sio lazima kila mshukiwa aachiliwe kwa dhamana.

Bw Ondari alisema ni mahakama tu iliyo na uwezo wa kutwaa haki za mshtakiwa za kuachiliwa kwa dhamana.

Bw Ondari alimweleza Jaji Lessit kuwa amewasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kumnyima dhamana.

Mawakili Cliff Ombeta, Jaji mstaafu Nicholas Ombija na Rogers Sagana wanaomwakilisha Bw Obado waliomba aachiliwe kwa dhamana wakisema ni haki yake na hakuna namna DPP anavyoweza kukaidi haki ya gavana huyo kuachiliwa kwa dhamana.

Mawakili hao walieleza korti kuwa hakuna ushahidi wowote uliowasilisha kuonyesha Bw Obado amefanya chochote kuwatisha ama kuvuruga ushahidi tangu kifo cha Sharon kitokee mnamo Septemba 3, 2018.