Simanzi mwanamume kufariki baada ya kuangukiwa na mwamba
BENSON AMADALA na CHARLES WASONGA
MWANAMUME mmoja Jumatano alifariki baada ya kuangukiwa na mwamba ambao alikuwa akijaribu kuchimbua katika boma moja katika kaunti ya Kakamega.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 30 alitambuliwa kama Stephen Ngaira. Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Kambi ya Mwanza, kaunti ndogo ya Kakamega Kaskazini.
Shahidi mmoja, Nelson Sakwa, alisema mwanamume huyo, na wenzake wawili, walikuwa wakichimba shimo na kutoa mchanga kando ya mwamba huo kisa hicho kilipotokea.
Mmoja wa wachimbaji wenzake waliponea japo akapata majeraha madogo.Mke wa mwenye boma hilo alikataa kutoa maelezo zaidi kuhusu kisa hicho akisema ni mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kuondoa mwamba huo ndiye angetoa maelezo hayo.
“Sikuwepo wakati wa tukio. Tafadhali ongea na mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kuchimbua mwamba huo na kuiondoa kutoka boma hili,” mwanamke huyo, ambaye alidinda kujitambua kwa jina, alisema.
Mwili wa mwendazake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maitti cha Hospitali ya Rufaa ya Kakamega. Maafisa kutoka Idara ya Kushughulikia Majanga katika kaunti ya Kakamega walifika katika boma hilo na kuandikisha taarifa kutoka kwa mashahidi.
“Tulimsikia akilia na tukawaonya wenzake kutahadhari kwa sababu mwamba huo ulikuwa umeanza kubingiria. Kwa bahati mbaya mwamba huo ulimwangukia na kumuua papo hapo,” akasema Bw Sakwa.
Wasimamizi wa Kampuni ya Sukari ya West Kenya waliingia kati janga hilo na kutuma trakta ili kuinua mwamba huo ndipo wanakijiji wakaweza kutoa mwili wa mwanamume huyo.