• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
KAULI YA MATUNDURA: Kiswahili kinashuhudia mwamko mpya na wa kipekee kote duniani

KAULI YA MATUNDURA: Kiswahili kinashuhudia mwamko mpya na wa kipekee kote duniani

NA BITUGI MATUNDURA

MWAKA huu unaweza kutajwa kuwa ‘mwaka wa matumaini makuu’ kwa lugha ya Kiswahili si tu Afrika ya Mashariki na Kati ambapo lugha hii inazungumzwa na takriban watu wasiopungua 120 milioni, bali pia barani Afrika kwa jumla.

Katika makala haya, ninadai kwamba juhudi za kustawisha Kiswahili kimakusudi zimeanza kuonekana. Juhudi hizi bila shaka zitakivusha Kiswahili hadi ng’ambo ya pili kama mojawapo ya lugha muhimu ulimwenguni.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyokwisha kupita, matukio manne makuu yamekwisha kutokea – nayo yanaashiria kwamba kuna nguvu na kani mpya katika maendeleo ya Kiswahili.

Kwanza, mataifa ya Afrika Mashariki yameazimia kubuni Mabaraza ya Kiswahili katika kila nchi mwanachama. Tunafahamu fika athari ya hatua hii katika suala zima la sera ya lugha Afrika Mashariki.

Pindi mabaraza hayo yatakapobuniwa, serikali za nchi husika zitawajibika kutenga pesa au raslimali za kuratibu maendeleo ya Kiswahili.

Tukio la pili ni wito wa mwanasiasa wa Afrika Kusini – Julius Malema kwamba bara la Afrika linapaswa kuwa na lingua franca au lugha ya mawasiliano mapana. Bw Malema, sawa na wasomi kama kina Wole Soyinka, Chinua Achebe, Alamin Mazrui, Ali Mazrui, Mohammed Hassan Abdulaziz miongoni mwa wengine amekipigia kura Kiswahili kuchukua nafasi hiyo.

Tatu, Afrika Kusini ambayo ina takriban lugha 11 rasmi imeamua kufundisha somo la Kiswahili katika mtaala wake.

Waziri wa elimu katika nchi hiyo – Angie Motshekga alitangaza kuwa Kiswahili kimeidhinishwa kufunzwa kama lugha ya pili itakayofunzwa katika shule za umma, binafsi na huria. Hatua hiyo imekwisha kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri wa Elimi (CEM) nchini humo.

Kiswahili ndiyo lugha ya tatu barani Afrika inayozungumzwa na watu wengi baada ya Kiingereza na Kiarabu. Aidha, Wizara ya Elimu ya Zimbabwe imeazimia kuanzisha ufunzaji wa Kiswahili, Kichina, Kifaransa na Kireno katika mtaala wake mpya.

Nchi hiyo pia itatumia lugha za kiasili katika lugha za chekechea. Lugha ya Mandharin ndiyo ina wazungumzaji wengi zaidi nchini Zimbabwe. Waziri wa Elimu wa Zimbabwe, Dkt Lazarus Dokora alisema hatua hiyo pia itaimarisha mtaala wa elimu wa nchi hiyo.

Tukio la nne pale ambapo Chuo Kikuu cha Azerbaijan katika Jamhuri ya Azerbaijan – kimeanzisha Idara ya Masomo ya Masuala ya Kiafrika na kutoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kutuma maombi ya kuifunza lugha hiyo. Matukio haya yanaonesha kwamba kuna mwamko mpya unaokichangamkia Kiswahili ulimwenguni.

Wataalamu na wakereketwa wa Kiswahili wanapaswa kuitumia fursa hizi kukipigia debe Kiswahili ili kiafikie nafasi yake stahiki kama mojawapo wa lugha muhimu ulimwenguni. Kiswahili kinaendelea kupasua kingo zake na kusambaa kotekote. Hii ni lugha ya kilimwengu inayostahili kutazamwa karne hii.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka. [email protected]

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Wanahabari waepuke uchale katika usomaji...

WAMALWA: KNEC isiwabebeshe wachapa kazi kwa uadilifu mzigo...

adminleo