WAMALWA: KNEC isiwabebeshe wachapa kazi kwa uadilifu mzigo ambao si wao
NA STEPHEN WAMALWA
BARAZA la Kitaifa la Mitihani nchini (KNEC) limewahakikishia wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nne kuwa wako tayari kwa mchakato wa kusimamia na kusahihisha mitihani ya kitaifa ya mwaka huu. Wanafunzi 1,060,703 wanatarajiwa kuufanya mtihani wa KCPE huku wanafunzi 664,585 wakiandaa kwa mtihani wa KCSE.
KNEC inasema kuwa matokeo ya mitihani ya mwaka huu yatatolewa mapema zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana. Matokeo ya mtihani wa KCPE yalitolewa tarehe ishirini na moja mwezi wa Novemba huku matokeo ya mtihani wa KCSE yakitolewa tarehe 20 mwezi wa Desemba mwaka 2017.
Kwa miaka miwili iliyopita, baraza hili limejizatiti kurudisha hadhi yake hasa kuhusu visa vya wizi wa mitihani. Mikakati mbalimbali imewekwa kuhakikisha kuwa visa vichache tu vinaripotiwa kwa kulinganisha na ilivyokuwa miaka ya hapo awali.
“Baraza la kitaifa la mitihani nchini sasa linaweza kuaminika ukilinganisha na ilivyokuwa awali. Linaweza likategemewa katika kuupima uwezo wa kila mwanafunzi,” akasema waziri wa elimu Amina Mohammed.
Mgala muuwe na haki yake mpe. Licha ya dosari za aina yake kushuhudiwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, mengi yamefanywa kuboresha utendakazi wa KNEC.
Sawa na ilivyo kila mwaka, onyo limetolewa kwa wadau kuwa yeyeote atakayepatikana akishiriki wizi wa mitihani ataadhibiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria. Lakini si ajabu kwamba baada ya mikakati na tahadhari zote hizi, pataripotiwa visa vya wizi wa mitihani.
Visa vya aina hii vinapotokea, mtego wa panya huwashika waliyomo na wasiyokuwemo. Baadhi ya shule, walimu, maafisa wa usalama na wanafunzi wameadhibiwa kutokana na makosa ya wadau wengine.
Kesi zimefikishwa mahakamani kuhusu wizi wa mitihani na mahakama zimewaweka huru waliokuwa wamekashiwa baada ya uchunguzi kuonesha kuwa walikashifiwa visivyo.
Baadhi ya maafisa wa serikali wamepoteza kazi zao huku wanafunzi nyota za wanafunzi wengine zikizimwa kighafla kwa makosa haya ya kijumuiya. Miongoni mwao, wamo wanaoamini kuwa walipewa hukumu kwa makosa yaliyofanywa na watu wengine.
Ni dhahiri kuwa ni vigumu kwa mwanafunzi, kwa mfano, kujitenga na wizi wa mtihani hasa wizi huu ukiwa unafanywa chini ya usimamizi wa wanaohitajika kuuzuia. Wanapokamatwa, shoka la hukumu huwaangukia wote, ima alipenda kuiba au la.
Ni vyema kwa wanaohusika na mchakato huu wa mtihani kutahadhari ili wasijipate wakiubeba msalaba wa wengine. Hata hivyo, ni muhimu kwa KNEC kuweka mikakati itakayowalinda wale watakaokuwa waadilifu hata kama kosa litakuwa la kijumuiya.
Mwandishi ni mhadhiri wa Lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika, Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kigeni cha Tianjin, Uchina.