Habari Mseto

Onyo kali kwa wanaouza unga kwa zaidi ya Sh75

October 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GITONGA MARETE

WAZIRI wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ameonya wafanyabiashara wanaouza unga wa mahindi kwa bei ya juu kuwa watakamatwa na kushtakiwa.

Waziri alisema wafanyabiashara ni sharti wauze kilo mbili za unga wa mahindi kwa Sh75 huku akisisitiza kuwa hilo halitakuwa na mjadala.

“Tangazo la serikali kwamba kilo mbili za mahindi ziuzwe kwa Sh75 si ombi bali ni agizo. Watakaokiuka agizo hilo wataadhibiwa kisheria,” akasema Bw Kiunjuri.

“Hatutaruhusu Wakenya kupunjwa na viwanda vya kusaga unga wa mahindi na wafanyabiashara walaghai,” akaongezea.

Waziri Kiunjuri alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Meru wakati wa hafla ya siku ya Wazalishaji Maziwa ambapo alikuwa mgeni wa heshima.

Hata hivyo, agizo hilo la Bw Kiunjuri huenda likagonga mwamba kwani Kenya ni soko huru ambapo wafanyabiashara wanajiamulia bei ya bidhaa zao.

Wakulima wa mahindi kutoka baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa wamepinga agizo hilo la Bw Kiunjuri huku wakisema kuwa litasababisha kudorora kwa bei ya mazao yao.

Lakini waziri alishikilia kuwa kwa sasa mahindi yanauzwa kwa bei ya chini hivyo unga pia unastahili kuuzwa kwa bei nafuu.

Alisema hatua ya serikali kuweka bei ya unga inalenga kuhakikisha kuwa watumiaji wa unga wanalindwa dhidi ya wafanyabiashara walaghai wanaouza bidhaa hiyo kwa bei ya juu.

“Haiwezekani bei ya unga kuendelea kuwa juu ilhali gunia la mahindi sasa linauzwa kwa Sh1,600 kutoka Sh2,800,” akasema Bw Kiunjuri.

Waziri pia alisema serikali imeanzisha mikakati ya kuhakikisha kuwa wafugaji wa ng’ombe wanapewa vifaa vya kuhifadhi maziwa.

“Maziwa ni bidhaa inayoharibika kwa haraka ikiwa haitahifadhiwa vyema.”