Habari MsetoSiasa

Gavana lawamani kuzima mashindano ya urembo

October 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ALEX NJERU

GAVANA Muthomi Njuki wa Kaunti ya Tharaka-Nithi amelaumiwa vikali na madiwani kwa kukataa shinikizo za kuandaa mashindano ya urembo akishikilia kuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Kwa sasa, madiwani hao wanamtaka kiongozi huyo kuelezea sababu yake kufutilia mbali mashindano hayo ambayo yalianzishwa na mtangulizi wake, Bw Samuel Ragwa.

Kufuatia hayo, madiwani wameipa kamati husika siku 14 kuwasilisha suala hilo katika Bunge la kaunti.

Madiwani hao pia wamemlaumu gavana huyo kwa kuwatowashirikisha vijana katika uongozi wake, huku wakiapa kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa mashindano hayo yamerejeshwa. Walieleza kuwa hafla hizo hukuza talanta.

Lakini akijitetea dhidi ya madai hayo, Bw Njuki alisema kuwa hataogopa vitisho vyao, kwani lengo lao ni kujipatia mamilioni ya pesa kama marupurupu. Alisema kuwa badala yake, atatumia pesa hizo kwa masuala muhimu kama afya, maji na kuimarisha hali za barabara.

“Kuna mambo muhimu sana ya kufanya, badala ya kuandaa mashindano ambayo hayatawasaidia wananchi hata kidogo,” akasema Bw Njuki.

Aliwalaumu kwa kutumia visingizio vya kuinua hadhi za vijana kujitajirisha.