• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Hospitali zinakaribiana na polisi kwa ufisadi – Ripoti

Hospitali zinakaribiana na polisi kwa ufisadi – Ripoti

Na CECIL ODONGO

ASILIMIA 11.9 ya Wakenya hulipa hongo katika hospitali za umma nchini ili kupokea huduma muhimu za kimatibabu, kulingana na ripoti kuhusu ufisadi mwaka wa 2017 iliyotolewa jana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Hospitali za umma zilikuwa katika nafasi ya tatu kwa ufisadi, nafasi ya kwanza ikishikiliwa na idara ya polisi wa Kenya (asilimia 23.8) na ya pili ikiwa ni Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (asilimia 13.7).

Katibu Mkuu wa Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi, Bw Seth Panyako, alisema itakuwa bora zaidi ikiwa EACC itafanya uchunguzi wa kina na kupata ushahidi wa kuwafungulia mashtaka wahusika katika vitendo hivyo vya ufisadi wakiwemo wakuu katika afisi kubwa zinazosimamia afya ya umma.

“Sikatai hakuna ufisadi katika sekta ya afya ila iwapo watampata muuguzi au daktari akishiriki ufisadi, mbona watangazie umma kila mara bila kuwachukulia hatua na kuwafikisha mahakamani? Yao ni hekaya na nimewaitisha ripoti hiyo ili nisome kabla ya kutoa kauli zaidi,” akasema Bw Panyako wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Vile vile ripoti hiyo iliyozinduliwa katika jumba la mikutano la KICC, Nairobi, imeitaja Kaunti ya Wajir kama inayoongoza katika visa vya wananchi kutoa mlungula kabla ya kupata huduma kwa asilimia 90.

Kaunti zilizofuta ni za Meru (asilimia 88.5), Trans Nzoia (83.3), Kajiado (asilimia 81.5), Kirinyaga (asilimia 81.3), Busia (asilimia 80.9), Makueni (asilimia 80.0), Nyandarua (asilimia 80.0), Bungoma (asilimia77.6) na Nakuru (asilimia 77.2).

Hata hivyo gatuzi la Bomet ndilo linaonekana maafisa wake hawana tamaa ya mlungula baada ya visa vichache kushuhudiwa katika kaunti hiyo kwa asilimia 24.1.

Kulingana na ripoti hiyo zaidi ya nusu ya raia waliotoa hongo walikubali kwamba hawakuwa na njia nyingine za kukumbatia ila kutoa kitu kidogo ndipo wapokezwa huduma, asilimia 17 wakasema ni njia ya kuharakisha utoaji huduma, asilimia 13 wakakubali ilikuwa mbinu ya kukwepa vita na waliopo uongozini kisha asilimia 10 wadai ni hali ya kawaida waliyoizoea.

Ilipatikana shughuli inayovutia utoaji hongo zaidi ni upeanaji wa zabuni kama vile za ujenzi wa miundomsingi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Halakhe Waqo akizungumza wakati wa kutolewa kwa ripoti hiyo, alisema kwamba tume hiyo ilishughulikia kesi 49 na kati ya hizo watu 39 tayari wameshtakiwa mahakamani.

Kulingana naye, hiyo ilikuwa hatua kubwa ikilinganishwa na 25 zilizoshughulikiwa mwaka jana na watu 17 kushtakiwa na kuhukumiwa.

You can share this post!

Isaac Ruto amkosoa Raila kwa kushirikiana na Uhuru

Majonzi washirika 5 wa kanisa moja kuangamia ajalini...

adminleo