Habari Mseto

EACC: Gazeti la Taifa Leo linaenziwa kwa kuchapisha taarifa za uhakika

October 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL oDONGO

GAZETI La Taifa Leo limeibuka la tatu kama gazeti linaloenziwa na kusomwa zaidi nchini nyuma ya Gazeti la Nation na Standard, hii ni kulingana na ripoti iliyotolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu vyombo vya habari vinavyong’aa zaidi katika tasnia ya uanahabari.

Taifa Leo ilizoa asilimia 5.5 nyuma ya Standard (asilimia 18.7) na Daily Nation kwa asilimia 47.0. Magazeti ya Daily Nation na Taifa Leo humilikiwa na kampuni ya Nation Media Group.

Katika kile kinachoonyesha mapenzi ya wananchi kwa Taifa Leo ambalo habari zake huwa kwa lugha ashirafu ya Kiswahili pekee, wengi wa waliohojiwa waliamini kwamba gazeti hili huwa limesheheni taarifa za kweli, za uhakika na zinazokemea maovu katika jamii kama ufisadi na dhuluma za kijamii.

Gazeti la The People Daily ambalo lilikuwa mpinzani wa karibu wa Taifa Leo lilishikilia nafasi ya nne kwa asilimia 0.8, The Star ikafuata kwa asilimia 0.4, Alternative press ikaibuka na asilimia 0.3, Kenya Times ikajihakikishia asilimia 0.2 kisha magazeti mengine yakagawana asilimia 27.1 jumuishi.

Habari hizi nzuri zinajiri wakati Taifa Leo linaadhimisha miaka 60 ya uwepo wake katika tasnia ya uanahabari nchini huku likiendelea kuwa gazeti la pekee la Kiswahili linashabikiwa taifa zima.

Kwa upande wa Runinga, Runinga ya NTV ambayo pia inamilikiwa na NMG iliibuka ya tatu kwa asilimia 8.8 nyuma ya Runinga za KTN na Citizen kwa asilimia 20.9 na 40 mtawalia.

Hata hivyo vituo vya radio vya lugha za mama vinapendwa zaidi na Wakenya kwa asilimia 36.6 huku Radio Citizen, Jambo na Maisha zikifunga orodha ya tatu bora kwa asilimia 20.3, 9.3 na 7.5 mtawalia.