Habari Mseto

Raia wa Mali na Mkenya ndani kwa kunaswa na Sh1 bilioni feki

October 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wawili wa kutoka nchi ya Mali iliyoko Afrika Magharibi na raia wa Kenya Jumanne waliamriwa wazuiliwe kwa  siku 15 kuchunguzwa walikotoa pesa feki Sh1 bilioni.

Mabw Abdoulaye Tamba Kouro na Abdalla Tamba wote kutoke nchi ya Mali walifikishwa mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Sinkiyiani Tobiko pamoja na Bw Antony Mwangangi Munyiva.

Kiongozi wa mashtaka aliomba hakimu aliamuru washukiwa hao watatu wazuiliwe katika vituo vitatu vya Polisi vya Kilimani , Kileleshwa na Pangani wawasaidie maafisa wa polisi wanaowahoji.

“Naomba hii mahakama ikubalie polisi wawahoji washukiwa hawa kwa muda wa siku 15. Ripoti nyingi zimetolewa na umma kuhusu watu wanaosambaza kwa matumizi pesa feki. Wamewatapeli watu wengi,” akasema kiongozi wa mashtaka.

Hakimu alifahamishwa kuwa watatu hao walitiwa nguvuni katika mtaa wa Lower Kabete katika majumba ya makazi ya Sandalwoods Apartments mnamo Oktoba 1, 2018.

Kachero Mohamud Godana Hussein anayechunguza kesi hiyo alimweleza Bi Tobiko kuwa anahitaji muda wa siku 15 kuwahoji kwa undani washukiwa hao kubaini vitu kadhaa.

“Nahitaji kutambua uraia wa Mabw Kouro na Tamba. Hawajaeleza kwa ukamilifu uraia wao na waliokotoa mabunda hayo ya pesa za kigeni zinazofanana na Dola za Kimarekani na sarafu za Euro,” alisema Konstebo Kouro.

Washukiwa hao walikutwa wamehifadhi katika makazi yao sarafu feki zilizofanana na dola za kimarekani na Euro za Ulaya.

Mahakama ilielezwa uchunguzi huo unalenga kuwatia washukiwa wengine nguvuni wanaoendelea kusakwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai.

Pia hakimu alifahamishwa polisi wanataka kuchunguza uraia wa washukiwa hawa kutoka Afrika magharibi.

“Nataka kuwasiliana na Benki Kuu ya Kenya (CBK) kubaini ikiwa makaratasi yanayofanana na dola za kimarekani na Euro ni halali au ni feki,” anasema Kachero Hussein.

Washtakiwa walipinga wakizuiliwa kwa siku hizo 15 wakidai ni nyingi lakini hakimu akasema “polisi wanahitaji muda wa kutosha kukamilisha zoezi hilo la uchunguzi na kutambuliwa kwa washtakiwa na walalamishi wanaodai walifujwa.”

Watarudishwa kortini Oktoba 19.