• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Densi za usiku kupigwa marufuku kwa kuathiri elimu

Densi za usiku kupigwa marufuku kwa kuathiri elimu

NA FADHILI FREDRICK

POLISI wa eneo la Msambweni Kaunti ya Kwale, wamesema watapiga marufuku sherehe na ngoma za usiku ili kuwazuia watoto wa shule kuhudhuria sherehe hizo.

Sherehe hizo ambazo ni harusi na ngoma za usiku, zinadaiwa kuchangia pakubwa kudorora kwa viwango vya elimu na matokeo duni ya mtihani.

Msaidizi wa kaunti kamishna wa Kwale (ACC) eneo la Msambweni Lucy Ndinda alieleza kwamba sherehe hizo za usiku zimekithiri mno eneo hilo na wanaoathirika ni wanafunzi wa kike ambapo hutungwa mimba za mapema.

“Tutapanga na washikadau wengine kuona ni jinsi gani tutaweza kushirikiana kupiga marufuku sherehe za usiku ili kuwanusuru wanafunzi wasiweze kupoteza nafasi zao za kimasomo kwa maisha yao ya baadaye,” akasema.

Viongozi wa serikali wanashutumu wazazi kwa kuwatelekeza na kuwaruhusu watoto wao kuhudhuria harusi na ngoma za usiku na kuliweka jambo hilo kama la kawaida.

Afisa wa utawala katika eneobunge la Msambweni Bw Hamisi Mwandaro alikashifu vikali hatua hiyo na kusema kwamba inaathiri pakubwa viwango vya elimu.

Hata hivyo, Mwandaro alisema kwamba suala hili linaweza kutatuliwa iwapo wazazi na viongozi watakaa chini pamoja na kujadiliana ili kupata suluhisho mwafaka.

Alisema jamii inapaswa kusimama imara kwa maovu ambayo yanaweza kuharibu watoto, kwani yasipodhibitiwa mapema kuna hatari kubwa ya kupoteza mwelekeo wa kizazi kizima.

Kauli hiyo iliungwa mkono na afisa wa elimu eneo la Msambweni Ahmed Mohammed ambaye alifichua kwamba kuna visa vya wasichana kudhulumiwa na wavulana japo wazazi hawapigi ripoti kwa maafisa wa polisi.

You can share this post!

Bangi ni hatari kwa akili za watoto – Utafiti

Mbunge akimbilia polisi baada ya kutwangwa na mkewe

adminleo