Habari Mseto

Mbunge akimbilia polisi baada ya kutwangwa na mkewe

October 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ERIC WAINAINA

WAPELELEZI wanafanya uchunguzi ili kujua ukweli kuhusu kisa ambapo Mbunge wa Githunguri, Kago wa Lydia, alipiga ripoti kwa polisi wa Kiambu akidai kutandikwa na mkewe Emily Wanjiku, ambaye pia aliwasilisha malalamishi sawa dhidi ya mumewe huyo.

Bi Wanjiku alidai kwamba mumewe alimpiga na kumjeruhi wakati alipomshambulia kwa vifaa mbalimbali ikiwemo pasi, ambapo aliumia shingoni, mgongoni na mikononi.

Picha kwenye mitandao zinamwonyesha mwanamke huyo akiwa na majeraha.

Kulingana na Bi Wanjiku, tukio hilo alilodai kutendeka Septemba 27 mwendo wa saa tano usiku, lilisemekana kusababishwa na ugomvi nyumbani kwao katika mtaa wa Five Star Estate, viungani mwa mji wa Kiambu.

Aliambia polisi wa Kituo cha Polisi cha Kiambu kwamba ugomvi wao uligeuka kuwa vita na ni wakati huo ambapo Bw Kago, alianza kumtia makofi, kisha akachukua pasi na kumchoma sehemu mbalimbali mwilini. Alitibiwa katika Hospitali ya Kiambu Level Five na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Lakini naye mbunge huyo aliwasilisha malalamishi mawili tofauti katika kituo cha polisi cha Kiambu akidai mkewe, ambaye ni mhudumu wa matibabu alikuwa amempiga.

 

UHALIFU

Mkuu wa kituo cha polisi cha Kiambu, Bw Patrick Kiprop, Alhamisi alithibitisha kuwa mbunge na mkewe walipiga ripoti katika kituo hicho na kuwa wapelelezi wanachunguza madai ya kila mmoja ili kufahamu ukweli.

Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai katika eneo hilo, Bw Paul Wambugu, alisema matokeo ya upelelezi wao ndiyo yatawawezesha kuamua kama watamshtaki mmoja wao au wote wawili. Alisema wanachukulia malalamiko hayo kama ya uhalifu.

Tulipowasiliana naye, Bw Kago alisema atatoa maoni yake baadaye kuhusu kisa hicho.

Kisa hicho kimevutia hisia mseto katika mitandao ya kijamii hasa Twitter huku wengi wakitilia mzaha.

Walioandika waliuliza iweje mbunge huyo alivyotandikwa ikizingatiwa anaonekana mwenye nguvu.