Habari Mseto

Kamaru alitaka kuishi miaka 120

October 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NDUNG’U GACHANE na WANDERI KAMAU

OMBI la mwanamuziki mkongwe Joseph Kamaru lilikuwa kuishi hapa duniani miaka 120.

Akiwa kitandani mwake, Bw Kamaru alimwomba Mungu kumpa miaka hiyo, ili kutimiza malengo yake ya kupanua sekta ya muziki nchini.

Hata hivyo, mauti yalimkumba akiwa na miaka 79.

“Najua kwamba hali yangu ya afya si nzuri, ila naomba Mungu kunipa muda wa kutosha kuniwezesha kutimiza lengo langu kuimarisha sekta ya muziki nchini,” akasema, siku chache kabla ya kifo chake.

Mzee Kamaru alifariki mnamo Jumatano usiku katika hospitali ya MP Shah, Nairobi, baada ya kuzidiwa na maumivu ya mifupa.

Mwanawe, Maina Kamaru, alisema kuwa marehemu alizidiwa na ugonjwa wa mifupa aliokuwa akiugua.

“Amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mifupa. Tunaamini hilo ndilo lilimzidia na kutuacha. Licha ya hayo, tunamshukuru Mungu kwa uhai wake,” akasema Maina.

Wakiomboleza kifo chake, viongozi mbalimbali na mashabiki wake wamesema kuwa kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa katika fani ya muziki kwenye jamii ya Agikuyu na nchi nzima kwa jumla.

Jana, Rais Uhuru Kenyatta aliwaongoza Wakenya kumwomboleza marehemu, akimtaja kama mwanamuziki aliyejaaliwa kipaji ambacho alitumia kuwafaa wanamuziki wengine.

Rais alisema kuwa Mzee Kamaru alitumia kipaji chake kuangazia maaadili katika jamii.

“Tulibarikiwa kama nchi kuwa naye, kwani alichangia pakubwa kuendeleza sekta ya muziki nchini. Tutakosa muziki wake, kwani ulijaa mafunzo na upekee mwingi,” akasema rais.

Naibu Rais William Ruto alitaja kifo chake kama pigo kubwa kwa mustakabali wa muziki nchini, akisema kuwa aliangazia maudhui muhimu ya kuifaa kila mwanajamii.

“Utunzi wake ulikuwa na upekee mkubwa, kwani uliangazia uhalisia wa kimaisha unaoikumba kila jamii. Namwomba Mungu aipe familia yake nguvu wakati huu mgumu wa kuomboleza,” akasema Bw Ruto.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga alimsifia kama “balozi wa muziki” ambaye kazi yake ilileta mageuzi makubwa kwa eneo la Kati na nchi nzima kwa jumla.

“Alikuwa mwanamuziki aliyewazungumzia Wakenya wote kwa nyimbo zake za kipekee,” akasema.

Alizaliwa mnamo 1939 katika eneo la Kangema, Kaunti ya Murang’a.

Safari ya mkongwe huyo ilianza mnamo 1965, alipojitosa rasmi katika tasnia ya muziki, miaka miwili tu baada ya Kenya kujinyakulia uhuru.

Kamaru alipata umaarufu kwa mara ya kwanza mnamo 1967, alipotoa wimbo ‘Celina’ ambao ulipokelewa vizuri sana na mashabiki wake. Baadhi ya nyimbo zake zilizofuata na kumtambulisha kama mwanamuziki wa kipekee ni ‘Muhiki wa Mikosi’ (Mpenzi wa Mikosi), Safari ya Japan (alioimba kumsifu Rais Mstaafu Daniel Moi), Tiga Kuheenia Igooti (Acha Kuidanganya Mahakama), Uthoni wa Mbaathii-ini (Uchumba Katika Basi) kati ya zingine.

Kijumla, alitunga nyimbo zaidi ya 2,000 zilizoangazia masuala ya utamaduni wa jamii ya Agikuyu, siasa, ndoa, mapenzi, ugonjwa wa Ukimwi kati ya mengine.

Wanamuziki wenzake pia walimsifia kama “baba yao” aliyewapa mwongozo mkubwa walipoingia katika uwanja huo.

Kulingana na mwanamuziki Epha Maina, Mzee Kamaru amefariki wakati akijitayarisha kuandaa mikakati ya kuwaunganisha wanamuziki wote katika ukanda wa Mlima Kenya.

Alisema kuwa marehemu alikuwa ashamtumia barua Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa ameahidi kumuunga mkono katika juhudi hizo.