Babaye Jacque Maribe ahofia maisha ya bintiye
GUCHU NDUNG’U NA NDUNG’U GACHANE
FAMILIA ya mwanahabari Jacque Maribe, imeeleza hofu ya maisha mwana wao kuwa hatarini, iwapo atakubali kutoa ushahidi dhidi ya mchumba wake, Joseph Irungu, ambaye ni mshukiwa mkuu kwenye kesi ya mauaji ya Monica Kimani.
Akizungumza na Taifa Leo, babake, Bw Mwangi Maribe alisema hawezi kumshauri bintiye kutoa ushahidi huo kwani kwa kufanya hivyo atakuwa akihatarisha maisha yake.
“Huenda Irungu hakutekeleza uhalifu huo peke yake. Ana uhusiano mpana na watu wasiofahamika vizuri. Washirika wake huenda wako huru na wanaweza kumdhuru binti yangu iwapo atakubali kutoa ushahidi dhidi yake. Anaweza pia kuishi na wasiwasi maisha yake yote,” akasema Bw Maribe.
Kumekuwa na habari kwamba huenda Jacque akakubali kutoa ushahidi dhidi ya mchumbake.
Bw Maribe pia alikiri kufahamu kuwa Irungu ni mchumba wa bintiye kwani amewahi kutembea nyumbani kwake akiandamana na bintiye mara mbili ama tatu, lakini hakujua kazi aliyokuwa akifanya.
“Jacque ni mtu mzima na sikuwa nikifuatilia masuala yake ya kimapenzi. Hata nilifahamu kuhusu kuchumbiwa kwake kupitia vyombo vya habari,” akaeleza Bw Maribe.
Lakini aliongeza kuwa uhusiano wa Jacque na Irungu haukuwa ukiendelea vizuri. Alieleza kuwa mnamo Septemba 20, siku moja baada ya Monica kuuawa, Jacque alikosana vibaya na Irungu katika baa. Aliongeza kuwa bintiye alitaka kumaliza uhusiano huo.
“Alimwambia Irungu amrudishie funguo za gari na kadi ya ATM. Walipofika nyumbani Jacque alitupa nje baadhi ya nguo zake. Alitishia kujiua iwapo Jacque angemwacha. Hapo ndipo alipojipiga risasi,” akasema Bw Maribe.
MALEZI YA JACQUE
Kwenye taarifa kwa polisi, Jacque kwanza alisema Irungu alipigwa risasi na majambazi lakini baadaye akasema alikuwa akijaribu kujitoa uhai.
“Huenda alisikitika kwa jaribio la mpenziwe kujiua. Wakati huo hakufahamu kuhusu Irungu kuhusishwa na mauaji ya Monica. Binti yangu hakuhusika katika mauaji ya Monica,” akasema babake.
Akaendelea: “Siku moja baada ya Monica kuuawa, binti yangu alisoma habari hizo katika Citizen TV. Anaweza kuwa na ujasiri kiasi gani ahusike katika mauaji na kisha aweze kusoma habari hizo. Sikumlea mwanagu jinsi hiyo.”
Nyumbani kwao katika kijiji cha Gathaithi, Kaunti ya Murang’a, wakazi wanamfahamu Bw Maribe kutokana na kuhusika kwake katika siasa, akiwa amewania kiti cha ubunge cha Kiharu mara mbili, lakini hawakuwa na habari Jacque anatoka kijijini mwao.
“Watoto hao walilelewa Nairobi. Tunamwona huyo Jacque kwenye televisheni tu lakini hatukujuwa ni wa familia hii,” akasema Eliud Mungai, mmoja wa wakazi wa Gathaithi.
Jacque, Irungu na Brian Kassaine wamo korokoroni wakisubiri kushtakiwa rasmi kuhusiana na mauaji ya Monica.