Joho aanzisha mikakati ya kuzima waasi katika ODM
MOHAMED AHMED na KAZUNGU SAMUEL
GAVANA wa Mombasa Hassan Joho ameanza kupanga mikakati ya kuzima nguvu za kisiasa za wabunge wa Pwani walioasi Chama cha ODM na kuanza kumpigia debe Naibu Rais William Ruto.
Mwishoni mwa wiki, Bw Joho alikutana na viongozi wa mashinani kutoka Kaunti ya Kwale wakiongozwa na Bw Omar Boga ambaye ni hasimu wa mbunge wa Msambweni Suleiman Dori.
Bw Boga ni katibu mtendaji wa chama cha ODM katika kaunti hiyo na alishindwa katika kura ya mchujo wa vyama na Bw Dori ambaye ni miongoni mwa wabunge waasi.
Mkutano huo uliofanyika katika afisi ya Bw Joho, umedhihirika kuwa mwanzo wa mipango ya Bw Joho kupambana na waliosaliti ODM katika eneo la Pwani.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na kiongozi wa kiislamu wa Kwale, Sheikh Amir Banda, ambaye pia ni mshawishi wa siasa za eneo hilo. “Sio siri tulikutana ili tuweze kujipanga na kiongozi wetu kwa maana watu wa Msambweni na Kwale kwa jumla tumekuwa mayatima. Tulimwendea Bw Joho kwa sababu yeye ni kiongozi wa Pwani mwenye uwezo wa kusaidia watu wake,” akasema Sheikh Banda.
Kwenye mitandao ya kijamii, Bw Joho aliutaja mkutano huo kama mwanzo mpya wa kusuluhisha matatizo ya wakazi wa Msambweni na Pwani kwa jumla hususan yale ya kisiasa.
Wakati huo huo, Mbunge wa Kilifi Kaskazini Bw Ken Chonga jana alikana madai kwamba yuko katika kundi linalomuunga Ruto kuwania Urais 2022.
Huku hayo yakijiri, Mwanasiasa mkongwe wa Pwani Bw Hassan Chitembe, ambaye ni mwenyekiti wa vuguvugu la Ngumu Tupu Handshake, alimtaka wabunge wa Pwani waache kumdharau Bw Joho na kinara wa ODM Bw Raila Odinga.
Matamshi ya Bw Chitembe yanajiri siku moja tu baada ya wabunge watatu washirika wa karibu wa Raila na Joho kudai kwamba wanaomwandama Ruto wanafanya hivyo kwa maslahi yao.
Wabunge hao walikuwa ni pamoja na Bw Teddy Mwambire (Ganze), Omar Mwinyi (Changamwe) na Mishi Mboko (Likoni).
“Hawa wanamfuata Bw Ruto kwa maslahi yao binafsi lakini ukweli ni kuwa maji yakizidi unga, watarudi tena nyumbani katika ODM.
Miaka ya nyuma, waliokuwa wabunge, Gedion Mungaro, Dan Kazungu, Mustapha Idd na hata Aisha Jumwa waliasi lakini baadaye Bi Jumwa akarudi tena alipoona mambo ni mazito,” akasema Bi Mboko.
Bw Mwinyi alisema kuwa wabunge hao wanajiridhisha mioyo yao kwa kusema kuwa naibu huyo wa Rais ataungwa mkono Pwani.