KURUNZI YA PWANI: Nyuki sasa watumiwa kupambana na mavamizi ya ndovu
NA BRIAN OCHARO
TATIZO la wanyama kuingia katika mashamba ya watu katika kaunti ya Taita Taveta limekuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo kwa miaka mingi.
Mgogoro kati ya wanyama pori hususan ndovu na wakazi hao limefanya watu wengi kupoteza maisha, kujeruhiwa na mimea yao kuharibiwa.
Kulingana na takwimu kutoka kwa Kamati ya Fidia ya Wanyamapori ya kaunti hiyo, eneo hilo lina kesi zaidi ya 20 ya vifo vinavyotokana na wanyamapori, majeruhi 235 na kesi 452 za uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo, simba, nyati na mamba.
Ili kutatua tatizo hili, wakulima katika eneo la Kajire wameamua kuzindua mbinu mpya ambayo wana imani itasaidia kupambana na ndovu waharibifu.
Wakulima hao wameanza miradi ya kuweka mizinga ya nyuki katika ukingo wa mashamba kwa maeneo ambayo ndovu wengi wanatumia kuingia katika shamba na makazi ya wanakijiji
Wanapanga kuweka zaidi ya mizinga 30 kwa mashamba ambayo yana uzoefu wa kuvamiwa na ndovu.
Bw James Makeo ambaye ni mkulima katika eneo hilo ambalo limepakana na Mbuga ya Wanyama ya Tsavo anasema kuwa wamekuwa wakipoteza mimea yao kutokana na uharibifu unaosababishwa na ndovu.
“Kumetokea vifo kadhaa, mimea yetu imeharibiwa sana na ndovu , hivi majuzi mwanamke mmoja alipigwa na butwaa na akafa baada ya kuona ndovu wengi wakiingia kwenye makazi yake,” alisema.
Anasema wameamua kutatua shida kama hizi na kuhakikisha kwamba ndovu hao hawafiki kwenye makazi ya watu n ahata shambani.
“Ni kwa sababu hii ndio tukaona ni afadhali tutafute mbinu ambayo itatusaidia na pia kuhakikisha kuwa ndovu wako salama,” alisema.
Abdurrahman Farouk ambaye anaongoza mradi wa kuweka mizinga katika njia zote zinazotumiwa na ndovu anasema ana Imani kuwa miradi hiyo itaafikia malengo yake.
“Nia yetu hasaa ni kusaidia kaunti nzima ili kila mahalai tuwawekee mizinga ili tutatue hii shida mara moja,” alisema. Kundi hilo linasema shuguli hiyo itaendelea katika maeneo ya Sagala. Kasigau, Bura Maktau na Taveta.
Bw Farouk anasema kundi hilo pia lina pania kuweka mizinga katika kaunti zote ambazo zinapakana na mbula la Wanyama la Tsavo ili kuleta amani kati ya binadamu na wanyamapori.