• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Kioja pasta kusaka tiba kwa mganga

Kioja pasta kusaka tiba kwa mganga

Na DENNIS SINYO

Kaimosi, Vihiga

WAUMINI wa kanisa moja eneo hili walimlaumu mke wa pasta wao kwa kumshawishi mumewe wampeleke mtoto wao mgonjwa kwa mganga.

Inasemekana mtoto huyo alikuwa ameugua kwa muda mrefu bila kupona. Yadaiwa alikuwa amepelekwa hospitali nyingi huku hela nyingi zikitumika lakini hakupona. Baadhi ya washiriki walitaka kufanya maombi maalum kutafuta nafuu.

Hata hivyo, mke wa pasta alipinga wazo hilo akisema kwamba alikuwa akijua aina ya ugonjwa ambao mtoto alikuwa akiugua. “Mimi ninajua huu ugonjwa. Si ugonjwa wa kupelekwa hospitalini, tiba ni kutafuta mganga kutatua shida hii,” alisema mama huyo.

Duru zasema kwamba mama huyo alimshawishi pasta kwamba wampeleke mtoto kwa mganga kwa madai mtoto alikuwa amefanyiwa mazingaombwe na watu wenye jicho mbaya na njia ya kumwokoa ilikuwa tu kutafuta huduma za mganga.

Yasemekana pasta alikubali ushauri wa mkewe ampeleke mwanawe kwa mganga mmoja mtaani humu. Mtoto alipohudumiwa na mganga afya yake ilidorora hata zaidi.

Hali hiyo iliwakera sana baadhi ya washiriki waliolaani kitendo hicho. Walidai kwamba mama huyo alikuwa amefanya makosa makubwa kumpeleka mtoto kwa mganga badala ya kumuombea.

“Kwani imani yako iko wapi wewe mama? Badala ya kuongoza maombi maalum, unakuwa wa kwanza kumbeba mtoto wa pasta wetu kwenda kuinamia mganga?” alifoka mshiriki mmoja.

Walikemea kitendo hicho huku kila mtu akitaka mama huyo aondolewe kwenye kanisa lao. Hali ya mtoto huyo ilipozidi kuwa mbaya, washiriki walimrejesha hospitalini na hata kuandaa maombi maalum kumwombea.

Baadhi ya waumini walianza kufunga na kuombea uponyaji wa mtoto na afya yake ikaimarika.

…WAZO BONZO…

 

You can share this post!

TAHARIRI: Sikukuu ziwe zenye manufaa kwa taifa

MOI DEI: Rungu ya Nyayo ilipoanguka na kuvunjika

adminleo