Habari Mseto

Makosa mengi yaliyosababisha vifo Fort Ternan

October 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na ANITA CHEPKOECH

WASAFIRI kwenye basi ambapo watu 55 walikufa katika eneo la Fort Ternan, Kaunti ya Kericho Jumatano alfajiri, walikuwa wamelalamika mara nyingi kuhusu kuendeshwa kwa basi hilo kiholela, kasi iliyozidi na kubeba abiria kupita kiasi.

Baadhi ya wasafiri ambao walinusurika kifo kwa tundu la sindano walieleza Taifa Leo kuwa basi hilo lilikuwa na wahudumu wajeuri, ambao waliwatusi abiria kila walipolalamika kuhusu basi hilo kuendeshwa isivyofaa.

Walisema ujeuri wa dereva na makanga wake ulianza walipofika Westlands, viungani mwa jiji la Nairobi mwendo wa saa kumi na mbili jioni, ambapo basi liligeuzwa na kurudi kituo cha mabasi cha Machakos kuchukua abiria zaidi, licha ya kuwa lilikuwa limejaa.

Polisi walisema basi hilo halikuwa na leseni ya kuhudumu usiku.

Kufikia jana jioni, watu 55 walikuwa wamethibitishwa kufa na wengine 16 walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali mbalimbali Kericho na Kisumu. Hii inaonyesha basi hilo lilikuwa limebeba abiria 71 badala ya 62.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Fort Ternan, kijiji cha Tunnel katika barabara ya Londiani – Muhoroni.

“Walijaza basi kupita kiasi. Watu wengine walikuwa wamekalia kreti za soda kwenye sehemu ya watu kupitia. Tulipolalamika, wahudumu walijibu kwa lugha chafu, wakati mwingine wakitwambia tununue magari yetu iwapo haturidhiki na usafiri wa umma,” akasema Bw Joseph Oponyo akiwa amelazwa hospitalini baada ya kujeruhiwa.

Alisema gari hilo lilikuwa likipoteza mwelekeo barabarani mara kwa mara na abiria walipomtaka dereva kupunguza kasi aliwapuuza. Walisema dereva huyo alionekana kukomaa kiumri.

Alisema walipofika eneo la tukio, basi lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi na wateja walikuwa wakipiga nduru hadi lilipopoteza mwelekeo na mara moja kimya kikaingia.

Wakati wa ajali hiyo, paa ya basi iling’oka huku na abiria wakarushwa nje na wengine kubanwa ndani ya gari kadri lilivyobingiria kwa umbali wa mita 20.

Watu 35 waliripotiwa kufariki papo hapo, huku wengine 20 wakidhibitishwa kufa walipofikishwa katika hospitali.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kericho, James Mugera alisema basi hilo la wateja 62 kwa jina ‘Home Boyz’ na linalomilikiwa na kampuni ya Western Cross Express, lilipoteza mwelekeo lilipokuwa likiteremka eneo la mlima, likagonga mabati kando mwa barabara na kubingiria hadi shamba lenye mawe.

Wakazi walisema walisikia honi zilizofuatana, mayowe kutoka kwa abiria na mlio mkubwa muda mfupi kabla ya tukio hilo, katika eneo ambalo walisema wameshuhudia ajali 20 katika kipindi cha mwaka mmoja. Walieleza kuwa hiyo ndiyo ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea eneo hilo.

“Wakati nilisikia mlio, nilifahamu kuwa hiyo ni ajali nyingine. Nilikimbia eneo hilo na kumpata abiria ambaye aliponea na akaniomba maji. Mwingine kando yake alikuwa akilia kisha vilio vikaanza kutokea sehemu tofauti. Niliamua kumsaidia mtoto ambaye alikuwa akivuja damu sana kichwani kwanza,” akasema Bw Jackson Kosgei, mkazi wa eneo hilo.