KURUNZI YA PWANI: Mahangaiko ya wakazi kuhusu kivuko cha Mtongwe
Na HAMISI NGOWA
TANGU kutokea mkasa wa kuzama kwa feri katika kivuko cha Mtongwe yapata miaka 24 sasa, huduma za uchukuzi wa Feri katika kivuko hicho zimekuwa zikiendelea lakini si za kutegemewa na wakazi jinsi ilivyokuwa kabla ya mkasa huo.
Katika siku za hivi karibuni,wakuu wa Shirika la Huduma za Feri (KFS), wamekuwa wakijaribu kutuliza joto la wakazi wa eneo hilo wanaliolilia kurejeshwa kwa huduma za feri kwa kutoa hakikisho la kurejeshwa kwa huduma hizo ambazo hutolewa kwa kipindi kifupi kabla ya kukatizwa.
Kukosekana kwa huduma za feri katika kivuko hicho, kumesambaratisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao kwa sasa wanaishi katika maisha ya uchochole.
Unapotembelea baadhi ya mitaa katika eneo hilo, taswira unayokumbana nayo ni nyumba zilizogeuka kuwa magofu na zingine kuwa mahame baada ya watu waliokuwa wamepangisha nyumba hizo kuhamia Likoni ili kuwa karibu na feri.
Watu wengi wamehamia eneo la Likoni ili kuepuka gharama ya nauli wanayotumia kila siku wanapotumia usafiri wa matatu na tuktuk wanapoelekea na kurudi kutoka kazini.
Kando na usafiri, hali ya maisha katika eneo hilo inasemekena kuwa ngumu kutokana na kusambaratika kwa biashara za baadhi ya wakazi ambazo wamekuwa wakizitegemea ili kuwakimu.
Hali hiyo imeonekana kuwa kero kubwa kwa wakazi wanaoishi katika eneo hilo ambao baadhi yao sasa wametishia kuelekea mahakamani ili kushtaki Shirika la huduma za Kenya feri ili liweze kushinikizwa kurejesha huduma hiyo.
Mzee Musa Bandari alisema Shirika hilo linafaa kuwafidia wakazi wa Mtongwe kutokana na kukosekana kwa huduma za feri licha ya kwamba wao ni walipa kodi kama wakenya wengine.
Alisema inasikitisha kuona wakazi wa eneo hilo wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma za feri hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuigiza feri moja iweze kuhudumu katika kivuko hicho.
“Wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozindua upya huduma za feri ya Mtongwe, alituhakikishia kwamba huduma hiyo haitasitishwa tena, lakini sasa twashangaa kuona mara huduma inapatikana mara nyengine tunamaliza miezi kadhaa bila ya kupata,” akasema.
Alisema kuharibika kwa baadhi ya feri katika kivuko cha Likoni haifai kutumiwa kuwa sababu ya kukosekana kwa feri katika kivuko cha Mtongwe akisema wakazi wa Mtongwe wamekuwa bila ya feri hata kabla ya kuharibika kwa feri hizo.
Lakini Bw Ali Sababu mzaliwa na mkazi wa Mtongwe anatofautiana na wazo la wakazi wenzake kutaka kulishtaki Shirika la huduma za feri akisema Shirika hilo linapitia kipindi kigumu baada ya feri mbili kuharibika.
Sasabu ambaye ni mwanachama wa kamati ya watu 20 inayowakilisha wakazi wa eneo hilo katika kufuatilia kinacholemeza kurejeshwa kwa huduma za feri eneo hilo, alielezea jinsi yeye pamoja na wenzake walivyojionea uhalisia wa mambo kuhusu tatizo hilo la feri.
“Najua tunapata shida kwa feri kuwa Likoni lakini kwa wakati huu ni vyema tuvumilie hadi wakati kutakuwa na feri za kutosha kwa sababu iwapo feri moja italetwa Mtongwe kutakuwa na msongamano mkubwa katika kivuko cha Likoni,’’ akasema.
Alisema wahudumu wa Kenya Ferry hawafai kulaumiwa kwa tatizo la feri katika kivuko cha Mtongwe jinsi baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanavyofikiria.
Alisisitiza kwamba iko haja ya usimamizi wa Shirika hilo kupewa nafasi hadi wakati ambapo kutakuwa na feri za kutosha kabla ya kupelekwa kwa feri katika kivuko cha Mtongwe.