TAHARIRI: Tulinde watoto dhidi ya maovu
NA MHARIRI
ZIMEBAKI wiki mbili pekee kabla ya kuanza likizo ya mwisho wa mwaka kwa wanafunzi katika shule za msingi na upili nchini.
Likizo hiyo imayotarajiwa kuanza Oktoba 27 huwa ndiyo ndefu zaidi kwa mwaka na wanafunzi watakaa nyumbani kwa zaidi ya miezi miwili.
Kinyume na miaka ya nyuma ambapo hofu pekee kwa wazazi ilikuwa mimba za mapema au kujiingiza katika utumizi wa dawa za kulevya, sasa hivi kuna mambo mengi yanayoweza kuwaharibu watoto. Miongoni na masuala ibuka hatari zaidi ni simu na michezo ya Kamari.
Kutokana na kuimarika kwa teknolojia, simu za kisasa ndio mtindo kwa karibu kila familia. Simu hizi mbali na mawasiliano, zimekuwa na manufaa makubwa kwa upande wa kuhifadhi, kutuma na kupokea pesa, kuimarisha uhusiano na pia kurahisisha mambo.
Lakini simu vile vile zina athari mbaya kwa wanaozitumia iwapo hawatakuwa waangalifu. Ni kwenye simu hizo ambapo kuna michezo inayoweza kuwafanya watu hata waamue kujinyonga.
Ni majuzi tu kuliripotiwa kisa cha vijana kujiua baada ya kucheza mchezo unaojulikana kama Blue Whale. Mchezo huo huwapa changamoto wanaoucheza kwamba wakamilishe hatua 50 katika kipindi fulani.
Hatua ya hamsini huwa ni kuwataka wanaoucheza wajitoa uhai kama wao kweli wanaamini kuwa mashujaa.
Pia ni kupitia mitandao kama vile Facebook na WhatsApp ambapo magaidi hutavuta watu wa kuwasajili katika makundi yao. Vijana huanza kuingizwa itikadi kali na hatimaye huchukua hatua ya kujiunga au kusaidia katika usajili wa wanachama wengine katika makundi ya kigaidi.
Wazazi wanapaswa kufahamu kwamba akili za watoto hazijapevuka na ni wepesi wa kuhaidawa.