Habari Mseto

Wakenya hulipa Sh9 bilioni kugharamia vifaa vya hospitali visivyotumika

October 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA hulipa Sh9 bilioni kila mwaka kugharamia vifaa vya hospitali ambavyo huwa havitumiki katika hospitali za kaunti.

Ripoti hii iliwasilishwa kwa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Makadirio Jumanne.

Mwenyekiti wa Tume ya Ugamvi wa Rasilimali (CRA) Jane Kiringai alisema hayo baada ya kufika mbele ya kamati inayoo ngozwa na Kimani Ichung’wa kutetea kuondolewa kwa Sh9.04 bilioni katika bajeti ya kaunti kutoka Sh314 bilioni, zilizokuwa zimetolewa awali.

Mwezi wa Septemba, Hazina ya Fedha iliondoa Sh55.1 bilioni katika bajeti ya kitaifa na serikali za kaunti kwa mwaka huu wa kifedha, katika hatua ya kupunguza matumizi ya fedha za serikali.

Hii ni kutokana na serikali kupungukiwa na mapato.

Kulingana na CRA, hatua hiyo ilitokana na mageuko yasiyotarajiwa katika mapato ya serikali. Awali, KRA ilikuwa imekadiria kukusanya Sh1.7 trilioni lakini makadirio hayo yakapungunzwa hadi Sh1.6 trilioni.

Oktoba 5, 2018, Rais Uhuru Kenyatta alitia sahihi mswada wa marekebisho wa fedha kwa lengo la kuongeza kiwango cha fedha kwa kaunti.

Kuhusiana na kuongezwa kwa bajeti ya vifaa vya matibabu kutoka Sh4.5 bilioni hadi Sh9 bilioni, Bi Kiringai alisema, “Tunakubali kuwa huu ni mzigo mkubwa kwa kaunti. Kufanya mambo magumu zaidi, baadhi ya vifaa huwa havitumiwi.”

Aliongeza kuwa hali hiyo walishuhudia katika kaunti za Isiolo, Siaya na Migori kutokana na hakuna wataalam wa kuhudumu na mashine hizo ambazo zitalipiwa hadi 2022.