• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Shahidi akana ushahidi dhidi ya Gavana Ojaamong

Shahidi akana ushahidi dhidi ya Gavana Ojaamong

Na RICHARD MUNGUTI

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya ufisadi dhidi ya Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong ulipata pigo kubwa Alhamisi baada ya shahidi muhimu kukana taarifa ya ushahidi.

Bw Nicodemus Mulako, ambaye ni katibu katika kaunti hiyo alimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti kuwa hakuandika taarifa yoyote ya ushahidi dhidi ya Ojaamong.

Bw Mulako aliambia mahakama kuwa “sikuandikisha habari yoyote kwa polisi dhidi ya Gavana Ojaamong.”

Baada ya kudokeza hayo mawakili James Orengo na Dunstan Omar wanaowakilisha washtakiwa waliomba mahakama itupilie mbali taarifa aliyotakiwa kuitoa kama ushahidi dhidi ya Gavana Ojaamong.

Mahakama ilimzima katibu huyo kutoa ushahidi ikisema, “hawezi kutegemea ushahidi ambao hakuhojiwa na kuuandikisha.”

Bw Mulako aliambia mahakama taarifa aliyotakiwa kutegemea iliandikwa Mei 7 2014 na wakati huo hakuwa ameajiriwa katika kaunti hiyo.

Bw Mulako alisema taarifa hiyo iliandikwa na katibu wa zamani katika kaunti hiyo.

Bw Ojaamong amekanusha shtaka la kufanya njama za kuifilisi kaunti hiyon Sh8milioni kwa kusikizana na kampuni ya Ujerumani kufanya utafiti kuhusu uteketezaji wa taka.

Ameshtakiwa pamoja na Bernard Yaite, Leonard Obimbira, Samuel Ombui, Allan Omachari na Edna Odhiambo.

Wanadaiwa walifanya njama hiyo kati ya Machi 15 na Septemba 25,2014. Mashtaka yasema mradi huo haukuwa umejadiliwa na kuidhinishwa.

Bw Ojaamong ameshtakiwa kuwa alifanya mashauri na kampuni ya Madam R Enterprise ya Ujerumani kufanya utafiti huo bila kuidhinishwa.

Bw Ojaamong alijadiliana na kampuni hiyo Aprili 7, 2014 akiwa jijini Berlin, Ujerumani.

You can share this post!

BIASHARA: Si haki serikali kuzuilia bidhaa za...

Raia wa Rwanda apatikana na hatia ya kumuua mwanamke...

adminleo