HabariSiasa

Uhuru na Raila kutuzwa London kwa kuzima uhasama wa kisiasa

October 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga watapokea tuzo ya heshima kuu nchini Uingereza kwa muafaka wao wa kumaliza uadui wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu.

Tangu walipoelewana mnamo Machi 9 baada ya chaguzi mbili za urais zilizosababisha mgawanyiko kitaifa mwaka uliopita na 2013, hali ya utulivu wa kisiasa imeshuhudiwa nchini.

Kutokana na mwafaka huo, wawili hao wameweka historia kwa kuwa viongozi wa kwanza wakuu wa Afrika kupokea tuzo ya ‘African Peace Award’ inayotambua kujitolea kwao kudumisha amani.

Tuzo hiyo itatolewa katika kongamano la siku mbili la kisiasa nchini Uingereza (London Political Summit) linalokamilka leo katika majengo ya bunge nchini humo.

Kongamano hilo lilifanyika katika mwezi ambapo Uingereza husherehekea watu wenye asili za Kiafrika wanaotoa mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali katika nchi hiyo. Sherehe sawa na hizo hufanyika pia katika nchi nyingine za magharibi ikiwemo Amerika na Canada.

“Ni heshima kuu kwetu kutuza viongozi hawa wawili shupavu kwa mwafaka wao wa amani uliokuwa wa kihistoria, ambao ulionyesha ukomavu na uvumilivu wa kisiasa,” waandalizi wa kongamano hilo walisema kwenye taarifa.

Tuzo hiyo imenuiwa kutambua mafanikio yaliyotokana na mwafaka huo kama vile kukomesha chuki za kikabila na ushindani wa kisiasa wenye dhamira mbaya, ufisadi serikalini na upotovu wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

Msemaji wa Ikulu ya Rais, Bi Kanze Dena alisema wanazo habari kuhusu tuzo hiyo ingawa hawajapokea mawasiliano rasmi.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Chama cha ODM, Bw Philip Etale alisema Bw Odinga atakubali tuzo hiyo japo hataweza kuhudhuria kongamano hilo Uingereza.

Jana Bw Odinga alikuwa Ethiopia ambapo alikutana na baadhi ya viongozi wa Sudan Kusini katika juhudi za kurudisha amani katika nchi hiyo.

Rais Kenyatta na Bw Odinga, walishangaza wengi walipoitisha kikao cha pamoja cha wanahabari Machi 9, ambapo walitangaza kuweka kando tofauti zao za kisiasa kwa manufaa ya kustawisha maendeleo yatakayosaidia kuinua maisha ya wananchi.

Hata hivyo, baadhi ya wandani wa kisiasa wa wawili hao bado hudai hadi leo kwamba lengo la Bw Odinga lilikuwa ni kujitafutia nafasi serikalini na kusukuma ajenda zitakazomwezesha kuingia mamlakani ifikapo 2022.

Katika Chama cha Jubilee, wanasiasa ambao hulalamika kuhusu mwafaka huo ni wandani wa Naibu Rais William Ruto, ambao wanaamini mwafaka huo ni njama ya kuvuruga mipango yake ya kumrithi Rais Kenyatta, ambaye anakamilisha hatamu yake ya pili na ya mwisho ya uongozi 2022.

Lakini Rais Kenyatta na Bw Odinga wameshikilia msimamo wao kwamba hatua waliyochukua ilikuwa muhimu kwa maslahi ya taifa lote.