Wakenya watuma na kupokea Sh1 trilioni kwa simu kwa miezi 3
Na BERNARDINE MUTANU
KWA mara ya kwanza, Wakenya wametuma, kulipa na kupokea zaidi Sh1 trilioni kupitia simu za mkononi katika robo iliyopita katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019.
Sh1.009 trilioni zilitumwa na kupokelewa kwa njia ya kidijitali ya simu katika muda wa miezi mitatu, kati ya Julai na Septemba 2018.
Hiyo ni Sh112.78 bilioni zaidi ikilinganishwa na kipindi kama hicho 2017.
Takwimu hizo zinamaainisha kuwa uchumi umeimarika nchini baada ya kipindi cha uchaguzi wakati ambapo Wakenya zaidi wameingia katika matumizi ya teknolojia.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya (CBK). Ripoti iliyotolewa inonyesha kuwa Wakenya walituma au kupokea Sh10.97 bilioni kwa njia ya simu kati ya Julai na Septemba 2018.
Katika kipindi kama hicho 2017, kiwango cha fedha zilizopitishwa kwa njia ya simu ni 9.74 bilioni, ilisema CBK.
Kulingana na CBK, huduma za rejareja, sekta ya kilimo na afya zinalipwa kwa njia ya simu kwani biashara zimeamua kuunganisha operesheni zake na huduma za simu.