Kitufe kipya kuwasaidia madereva wa Uber
Na BERNARDINE MUTANU
KAMPUNI ya Uber kwa lengo la kuimarisha usalama imezindua kitufe katika apu yake ya uchukuzi kwa lengo la kuwasaidia madereva kubonyeza kupata huduma za dharura moja kwa moja.
Kampuni hiyo ilisema kuwa hicho ni baadhi mikakati kabambe ya kuimarisha usalama itakayozinduliwa wiki chache zijazo Afrika, Mashariki ya Kati na Uropa.
Kidude hicho kinajumuisha nambari tano za mawasiliano ambazo wanaweza kushirikisha katika safari yao kupitia kwa apu hiyo.
Kina mahali pa kubonyeza wakati wa hali dharura kuchochea kampuni za usalama kuchukua hatua dereva anapojipata matatani.
Kituo cha usalama cha Uber kitakuwa na uwezo wa kupata habari kuhusu ziara ya dereva na gari, huduma za wateja na teknolojia ya kufuata liliko gari (GPS).
Madereva pia watapokezwa tahadhari na kidude hicho wakivuka kasi ya kawaida inayohitajika barabarani.
Pia, kidude hicho kinalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uaminifu kwa watumiaji wote.
“Kutokana na ziara zaidi ya 15 milioni kila siku kupitia Uber, hakuna kitu muhimu zaidi kuliko usalama wa madereva na wachukuzi,” alisema msimamizi mkuu wa usalama wa Uber ulimwenguni Sachin Kansal.