Wanafunzi sasa kujiunga na vyuo vya ualimu kwa alama ya D+
Na OUMA WANZALA
SERIKALI imepunguza alama za kujiunga na vyuo vya mafunzo ya walimu kwa wanafunzi kutoka kaunti 17 zilizo nyuma kimaendeleo.
Tayari wanafunzi kutoka kaunti zilizo nyuma kimaendeleo wamesajiliwa wakiwa na alama za chini kwa mafunzo ya ualimu ya vyeti na diploma.
Wizara ya Elimu iliwasajili wanafunzi hao licha Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kutaka sera iwekwe kabla ya kanuni mpya kuanza kutekelezwa.
Kwenye barua kwa Afisa Mkuu wa Tume ya Walimu (TSC), Nancy Macharia iliyoandikwa Oktoba 15, waziri Amina Mohammed alisema vyuo vya mafunzo ya walimu vitasajili wanafunzi walio na alama ya D+ mwaka huu.
Hata hivyo, alisema kuanzia mwaka ujao alama itakuwa C- kwa watakaosomea Diploma.
Kaunti ambazo zitafaidika ni Turkana, Samburu, Wajir, Marsabit, Isiolo, Mandera, Garissa, Lamu, Baringo, Narok, Kajiado, Kwale, Kilifi, Taita Taveta, Tana River na West Pokot.
Bi Mohamed alisema lengo ni kukabiliana na uhaba wa walimu katika kaunti hizo ambao alisema umeathiri viwango vya elimu.
Alama ya kujiunga na vyuo vya mafunzo ya awali ilikuwa ni C na C+ kwa waliosomea Diploma.
Hata hivyo, TSC imekataa mapendekezo hayo ikisema haitawatambua walimu hao.
Kwenye barua iliyoandikwa Septemba 25 kwa mkurugenzi ubora wa masomo Juma Mukhwana, Bi Macharia alisema kupunguza alama hizo kutaathiri viwango ya walimu.
Kulingana na TSC, mamlaka hiyo haifai kuamua alama za wanafunzi wanaojiunga na ualimu.
Bi Macharia alisema kama mwajiri wa walimu, ni tume yake iliyo na mamlaka ya kuweka viwango vya mafunzo kwa wanaotaka kujiunga na ualimu na kuishauri serikali ipasavyo.