• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Ulinzi waimarishwa KCSE ikianza

Ulinzi waimarishwa KCSE ikianza

Na VALENTINE OBARA

WANAFUNZI wa Kidato cha Nne wanaanza mitihani yao ya kitaifa (KCSE) Jumatatu huku wakionywa vikali dhidi ya udanganyifu.

Viongozi serikalini akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, na mwenzake wa elimu, Bi Amina Mohamed, wamekuwa katika mstari wa mbele kutaka kuwe na uaminifu katika mitihani hiyo huku wakionya yeyote atakayejaribu kushawishi wanafunzi kushiriki katika ulaghai.

“Tutaadhibu wale ambao wanajitahidi kuvuruga mfumo wetu wa mitihani. Hatima ya nchi hii inategemea watoto wetu. Tuko tayari kuwalinda kutoka kwa walaghai ambao wanataka kuharibu maisha ya watoto,” Rais Kenyatta alisema wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa wizara ya elimu, wanafunzi 664,587 wamepangiwa kufanya mtihani huo. Miongoni mwao ni wanafunzi 341,089 wa kiume na 323,498 wa kike.

Ili kusisitiza kwamba serikali haitavumilia wizi wa mitihani mwaka huu, Dkt Matiang’i alisema anashirikiana kwa karibu na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, Bw George Kinoti, na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji.

Mbali na haya, darubini italenga pia sehemu ambapo kumekuwa na usalama duni katika miezi michache iliyopita.

Shule kadhaa zilifungwa katika maeneo yaliyokumbwa na ghasia za kijamii kama vile kaunti ndogo za Narok Kusini, Narok Kaskazini, Molo, na sehemu za Mlima Elgon.

Mapema mwezi huu, Bi Mohamed aliambia Kamati ya Bunge inayosimamia Elimu kwamba watahiniwa waliokuwa wamesajiliwa katika shule hizo walitafutiwa vituo mbadala watakakofanyia mitihani yao.

Kwa upande wake, Dkt Matiang’i alisema wizara yake kupitia kwa idara ya polisi inayosimamiwa na Inspekta Jenerali Joseph Boinnet, itapeleka maafisa wa kutosha wa polisi kuimarisha usalama katika maeneo yaliyo na sifa za utovu wa usalama, yakiwemo maeneo yanayokumbwa na tishio la mashambulio ya kigaidi ya mara kwa mara kama vile kaunti zilizo Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Kulingana na wizara ya usalama wa ndani, kutakuwa na maafisa wa polisi zaidi ya 20,000 ambao watatoa ulinzi wakati wa mitihani.

Kama ilivyo kawaida, mitihani hiyo itafanywa katika msimu wa mvua za vuli ambazo hutatiza usafiri katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Ripoti ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa kuhusu msimu huu ambao huanza Oktoba hadi Desemba inaonyesha sehemu nyingi za nchi zitapokea kiwango kikubwa cha mvua kuliko kawaida, hasa mwezi ujao.

Maeneo hayo yako katika kaunti zote za Magharibi, Nyanza, Kati ikiwemo Nairobi, Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki na Rift Valley. Maeneo ya Mashariki ni Meru, Embu, Tharaka na Machakos, huku Pwani kukiwa ni Mombasa, Kilifi, Kwale, Lamu na sehemu chache za Tana River.

You can share this post!

Wanafunzi sasa kujiunga na vyuo vya ualimu kwa alama ya D+

Sonko adokeza hatatetea ugavana 2022

adminleo