Habari Mseto

Waziri atetea gredi ya D+ kwa ualimu

October 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

WAZIRI wa elimu Amina Mohamed ametetea hatua ya serikali kupunguza gredi za walimu wanaojiunga na vyuo vya mafunzo ya walimu, akisema kuwa ni sehemu ya kutetea maslahi ya jamii zilizoko maeneo magumu ili kuwe na usawa, kama inavyohitaji katiba.

Bi Mohamed amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo katika nchi ambayo si sawa na mengine, na hivyo yatahitaji kutumia huduma za walimu wa gredi hizo za D+ na C-, ambazo mbeleni zilikuwa za juu, japo akisema kuwa hatua hiyo haitashusha kiwango cha elimu maeneo hayo.

Akizungumza wakati wa kongamano la vyuo vikuu vya Afrika kuboresha utafiti na uzinduzi wa kiteknolojia, waziri huyo badala yake alisema kuwa serikali itatumia mbinu mwafaka kuhakikisha kuwa inaboresha viwango vya elimu, kwa misingi iliyopo.

“Pale ambapo hatuna ubora tunataka kuanza kuboresha kwani ili kuzungumza kuhusu ubora ni sharti tuwe na msingi fulani,” akasema.

Aliwakosoa wale wanaokashifu hatua hiyo kuwa itaharibu viwango vya elimu kuchunguza misingi iliyopo katika maeneo husika kabla ya kutupa lawama.

Bi Mohamed alisema kuwa maeneo ambayo yanapunguziwa gredi ni yale yaliyo na matatizo ya aina fulani ambayo yamekuwa yakiadhiri elimu.