Makala

TAHARIRI: Ripoti ya ufujaji pesa isipuuzwe

October 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

RIPOTI ya mhasibu Mkuu wa Serikali kwamba madiwani wamekuwa wakifuja fedha za walipa ushuru katika mabunge ya kaunti haifai kupuuzwa.

Kulingana na ripoti hiyo, madiwani wamekuwa wakitumia mbinu za udanganyifu kujipatia mamilioni ya fedha kupitia marupurupu ya kuhudhuria vikao vya kamati za bunge, safari za ndani na nje ya nchi.

Kwa mfano, ripoti hiyo inaonyesha kuwa madiwani wa Kericho walitumia jumla ya Sh187 milioni kuandaa vikao 1,159 katika mwaka wa matumizi ya fedha wa 2016/2017 uliomalizika Juni 30, mwaka huu.Katika vikao hivyo, madiwani wa Kericho walifanikiwa kuandaa ripoti 18 pekee.

Katika Kaunti ya Nyeri, madiwani walitumia jumla ya Sh128 milioni kujipatia marupurupu ya kusafiri na kuhudhuria vikao.

Madiwani wa Samburu walitumia kitita cha Sh56 milioni kuvinjari na kujilipa marupurupu ya kusafiri na kuhudhuria vikao.

Jambo la kuhuzunisha zaidi ni kwamba, baadhi ya madiwani wanalipwa kwa kuhudhuria vikao viwili kwa wakati mmoja. Je, hili lawezekana vipi?

Mnamo 2015, ripoti ya Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) ilifichua kuwa wabunge katika Bunge la Kitaifa wanatumia ulaghai kujipatia mamilioni kupitia marupurupu ya kusafiri katika maeneobunge yao.

Ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Spika wa Bunge Justin Muturi na kufikia sasa hakuna mbunge ambaye ameadhibiwa kwa kujihusisha katika wizi wa fedha za umma.

Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko, kama ilivyo kawaida, itatupwa na kusahaulika huku madiwani wakiendelea kuiba fedha kiholela.

Ugatuzi ulibuniwa kwa lengo la kustawisha maeneo yote ya Kenya, na fedha hizo zingetumiwa kununua dawa hospitalini, kutengeneza barabara na kuboresha elimu ya chekechea lakini zinaishia mifuko ya watu wachache. Hospitali nyingi zinazosimamiwa na serikali za kaunti pia hazina dawa na wagonjwa wanalala sakafuni.

Tume ya EACC na Idara ya Upepelezi (DCI) zinafaa kuchunguza kaunti zilizotajwa katika ufujaji wa fedha za umma ili wahusika wanaswe na kushtakiwa.

Maseneta hawana budi kutumia sheria hiyo kubuni sheria itakayoziba mianya hiyo inayotumiwa na madiwani kuiba fedha za umma.