• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kumbukumbu za mkasa wa ndege Ziwa Nakuru

Kumbukumbu za mkasa wa ndege Ziwa Nakuru

RICHARD MAOSI  NA  MAGDALENE WANJA

OCTOBA 21 mwaka wa 2017 habari za tanzia zilizagaa katika mitandao ya kijamii kuhusu ndege iliyotumbukia ndani ya Ziwa Nakuru.

Kutokana na ukosefu wa habari za kutosha kuhusu abiria waliokuwemo, duru za kuaminika zinasema  ajali hiyo ilitokea dakika chache baada ya kuondoka mjini Nakuru.Safari hiyo ikihusishwa na kikosi cha kampeni za Jubilee, waliokuwa wamekita hema katika mkahawa wa Jarika Nakuru.

Waling’oa nanga saa 6.00 asubuhi dakika 30 baadaye ndipo ajali ikatokea.

Helikopta ya 5Y-NMJ ilikuwa chini ya usukani wa Flex Air Charters kwenye juhudi za kufanikisha kampeni ya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka uliopita.

Baadaye ilifichuka kuwa ndege hiyo ilibeba watu 5:rubani Apollo Malowa,Sam Gitau,John Mapozi,Antony Kipyegon na Veronica Muthoni.

Kutokana na ukosefu wa vyombo vya usalama ziwani Nakuru,ililazimu kuagizia huduma za meli kutoka ziwa, Naivasha,jirani na hapo ili kuokoa hali.

Wiki ya kwanza wazamia majini walifanikiwa kupata miili ya manusura 2 kati ya 5 waliozama,vyombo kutoka idara ya serikali vikichangia pakubwa katika mchakato huo mzima.

Jamaa na marafiki wa watu walioangamia kwenye mkasa wa ndege Ziwa Nakuru Oktoba 21, 2017 wajumuika kwa hafla ya kumbukumbu. Picha/ Richard Maosi

Wizara ya Madini ilitoa wataalamu waliofika kuchunguza mabaki ya vyuma kutoka kwenye vifusi vya meli .Aidha wizara ya uvuvi ilitoa wazamiaji pamoja na mashua maalum kutekeleza uokozi uliofanya matumaini ya wengi kufifia.

Mabaki ya ndege yalipopatikana, ndipo  na maiti ya tatu ilikutwa imesakama katikati ya vifusi vyake.

Sio mwingine isipokuwa Veronica Muthoni,mwanamke wa pekee katika msafara huo.

Juhudi za kutafuta miili mingine mitatu hazikufua dafu kisha operesheni ikasitishwa rasmi na shughuli kuendelea kama kawaida.

Familia za John Mapozi na Sam Gitau hazikupata nafasi mwafaka ya kuwasindikiza wanao kwa njia iliyostahili.

Mwaka mmoja baadaye Bi Rahab Nyawira bado anaomboleza mchumba wake Gitau.

Wiki mbili baada ya mkasa huo Nyawira alijifungua mtoto wa kike aliyemwachia kumbukumbu tele kuhusu mumewe.

“Japo hatukuwa tumeweka wazi mahusiano yetu kwa wazazi,tayari tulikuwa tukiishi pamoja kama mume na mke chini yap aa moja,” Nyawira alisema.

Anakumbuka jinsi alipokea ujumbe huo wa mkasa na maisha yake yakabadilika kabisa kuanzia hapo.

Kuwakumbuka wapendwa wao walioangamia ajalini, wakazi wawasha mishumaa kwa pamoja. Picha/ Richard Maosi

“Nilikuwa nikitazama televisheni kuhusu habari za ndege iliyozama ziwani Nakuru ila sikutarajia kwamba mume wangu angekua miongoni waliohusika,”aliongeza Nyawira.

Dadake Gitau ndiye alimpigia simu na kumpasha habari hizo za taanzia kuhusu maafa yaliyofika familia hiyo changa.

Akiwa mwenye woga na wasiwasi alikimbia kwa mamake ambapo alipata habari kamili huku juhudi za kuokoa zikiendelea mwendo wa kobe.

“Sijawahi kupokea simu ya kushtua kama hii,na maisha yangu tena sio kama zamani,” Nyawira alisema.

Anakumbuka nyakati nzuri walipokuwa pamoja na mchumba wake, wakiahidiana mambo tele kuhusu ujauzito wake na mafanikio mengi siku za usoni.

“Nakumbuka ujauzito ulipofika miezi 5 aliwahi kusema binti yetu angewahi kukosa kitu chochote maishani mwake,” alisema.

Nyawira alitumia wakati wake mwingi akieleza wanahabari wa Nation kuhusu mipango yake ya siku za usoni,kuhusu familia yao iliyoendelea kua taratibu tangu apatane na mumewe.

“Akiwa mwandishi wa mtandaoni,alikuwa na ndoto ya kurejea chuoni,kusomea shahada katika ulingo wa siasa,ili agombee wadhifa 2022.Pia mimi nilitaka kufanya kozi ya pili,”alieleza

Bi Nyawira anasema lengo lake kuu hivi sasa ni kulea binti yao kama walivyoahidiana na mchumba wake akiwa hai.

Maswali mengi anayoibua anaonekana kunyoshea kidole cha lawama katika idara husika akishindwa kueleza ilikuwaje vigumu kupata maiti ya mumewe.

“Labda siku moja atarejea na kunikuta nikijikaza ksabuni kuhangaikia maslahi ya binti yetu mdogo.Hivi sasa anaomba serikali iweke wazi ripoti ya uchunguzi kuhusu mkasa wa ndege.

“Hatujui ni kipi kilitokea mwaka mmoja tangu mkasa huo kutendeka, tulipoteza wapendwa wetu katika mazingira ya kutatanisha kwa hili tunasononeka,” Nyawira alisema.

You can share this post!

Maafisa wa Kenya Power mashakani kuhusu kupotea kwa ushahidi

Mke alishwa talaka kwa kukosa kumakinika katika mapishi ya...

adminleo