Habari Mseto

Mke alishwa talaka kwa kukosa kumakinika katika mapishi ya pilau

October 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

MWANAUME kutoka Kaunti ya Tana River amemlisha mkwewe talaka kwa kumwaandalia visivyo mlo wa pilau unaohusudiwa sana katika jamii ya Waswahili.

Ndoa hiyo iliyodumu kwa mwaka mmoja unusu ilifikia ukingoni baada ya mwanaume huyo kuonja mlo huo na kuutema akisema si mtamu na haukupikwa vizuri.

Kulingana na mkewe, Mariam Hiribae, mumewe Said Kofa amekuwa akimwekea presha ili ampikie pilau ila amekuwa akichelea kufanya hivyo kwasababu hafahamu vizuri risipe ya kuandaa chakula hicho.

“Nimemwambia mara si moja kwamba kadri ninavyojitahidi kupika pilau ndivyo matokeo huwa kinyume, Nilihitaji muda zaidi wa kujinoa ila mara hii alikataa kunielewa na ikabidi nizamie upishi huo,” akasema Bi Hiribae.

Aidha alifafanua kwamba mara kwa mara amekuwa akitafuta huduma za marafiki ambao huanda pilau ya kudondoshewa mate na mumewe kwa malipo japo mara hii mzee wa watu alimtaka kuipika liwalo liwe.

Haya yalitimia baada ya bibi huyo kuomba risipe kutoka kwa jirani kisha akaanza mapishi naye mumewe kama askari langoni akaamua kupiga doria ili asipate usaidizi kutoka kwa mtu yeyote.

Baada ya muda wa saa mbili za shughuli za mapishi huku akifuata mwongozo wa mapishi kwa makini ya macho, Bi Hiribae alijishaua kwa mumewe kwamba amefanya kazi kuntu na kuandika meza kwa mlo wa pilau uliopikwa ukapikika.

Hata hivyo alitamani ardhi ipasuke immeze mzimamzima Bw Kofa alipotia chakula hicho mdomoni na kukimbilia maliwatoni akikohoa kisha kukitema kama shubiri akisema mkewe alitaka kumuua.

Haya yalifuatiwa na kofi kali na hasira za mkizi za mume huyo jambo lililomfanya Bi Hiribae kupandwa na za kwao na akachukua kiti kilichokuwa karibu kisha kumwangushia mumewe kipigo cha nguruwe msikitini kichwani.

“Tangu tuoane hajawahi kunielekezea kidole wala kunipiga lakini nilishangaa aliponilaumu kwa kupanga njama ya kumuua kwa kuweka viungo vingi katika chakula hicho. Nami nilishikwa na ghadhabu na kumpiga kichwani kwa kiti,” Bi Hirbae akasimulia.

Maji yalizidi unga mwanaume huyo alipotimka mbio na kuelekea kwa wakwe zake akiwaamrisha waje wamchukue mwanao huku akikimbia hospitalini kupokea matibabu kusimamisha damu nyingi iliyokuwa ikivuja kichwani.

Bi Hiribae baadaye jioni alielekea kwa wazazi wa mumewe ili kuwaeleza kilichotokea akiwa amebeba chakula hicho na kumkabidhi mamake mkwe akifanyie uchunguzi na kutoa kauli yake.

Cha kushangaza ni kwamba jaribio la mauaji lilipuuzwa na madai mengine ya kutokuwa mwaminifu kwenye ndoa, kuvaa mavazi yasiyohitimu mtihani wa maadili, kutowika chumbani wakati wa mahaba, kichwa kigumu miongoni mwa madai mengine.

“Nilishutuka sana kusikia kwamba mume wangu amekuwa akipiga ripoti na kuwambia wazazi wake kwamba nimekuwa nikiyatenda maovu hayo ambayo ni uongo tu. Ni kama wameamua hawanitaki tena,” akasema Bi Hiribae.

Siku iliyofuata, Bw Kofia akiandamana na dadake walirejea kwake na kumpa talaka jinsi inavyotakikana katika dini ya Kiislamu.

“Nilirejea nyumbani nikiwa na machungu. Bado sielewi kwa nini aliamua hivyo. Ninampenda na tuliishi kwa furaha lakini sikuwahi kufikiria mlo wa pilau ungetufikisha hapa,” akaongeza.

Alipofikiwa, Bw Kofa aliwaka na kusema hahitaji kutoa maelezo kwa yeyote kuhusu talaka hiyo kwasababu ni uamuzi alioufanya bila kushinikizwa na yeyote.

“Sihitajiki kutoa maelezo kwa yeyote kuhusu uamuzi ninaochukua katika maisha yangu. Umeoa? Una mtoto? Utakaa kwa ndoa hadi lini na mwanamke asiyeweza kujifungua mtoto na vile vile kukosa ujuzi wa kupika?,” akauliza akiwa amejawa na hasira za mkizi.

Hata hivyo kuna uvumi kwamba Bw Kofa alikuwa katika uhusiano na mwanamke mwengine aliyeletewa na mamake aliyekuwa na uja uzito wake. Talaka aliyopokezwa Bi Hiribae ilikuwa njia ya kuhakikisha wawili hao wanaoana.