MAPENZI MAHAKAMANI: Jacque na Jowie kujua hatima yao Oktoba 30
Na RICHARD MUNGUTI
KATIKA siku iliyojaa mapenzi na kukumbatiana mahakamani, mwanahabari Jacque Maribe na mchumba wake Bw Joseph Kuria Irungu watakaa rumande hadi Oktoba 30 mahakama kuu itakapoamua hatima yao ya dhamana.
Jaji James Wakiaga aliamuru wazidi kuzuiliwa katika idara ya magereza hadi mahakama itakapoamua ombi lao.
Mawakili Katwa Kigen na Wahome Thuku wanaomwakilisha Bi Maribe aliyekuwa ameajiriwa na kituo kimoja na televisheni kabla ya kutiwa nguvuni pamoja na mchumba wake kwa mauaji ya mwanamke aliyekuwa akifanya biashara nchini Sudan kusini.
Wawilli hao wameomba mahakama kuu iwaachilie kwa dhamana wakisema ni haki yao.
Bw Kigen alimweleza Jaji Wakiaga kuwa Bi Maribe amekuwa akishirikiana na polisi wanaochunguza mauaji ya Monica mnamo Septemba 16, 2018 katika makazi yake mtaa wa Kilimani.
Mahakama ilielezwa hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa na upande mwa mashtaka unaoongozwa na Bi Catherine Mwaniki.
Bw Ombeta alieleza mahakama kuwa Bw Irungu ni mzaliwa wa Kenya na makazi yake yanajulikana na Polisi.
Alisema wazazi wake hufika mahakama kila wakati kesi hiyo inapotajwa kufuata inavyoendelea.
“Bw Irungu hawezi kutoroka na atafika mahakamani atakapohitajika,” alisema Bw Ombeta.
Mahakama iliombwa isipotoshwa chungu nzima zilizochapishwa na vyombo vya habari kuhusu kesi hii.
Mahakama iliambiwa kuwa ushahidi ndio utakaotegemea ikiwa washtakiwa walihusika na mauaji ya kinyama ya Monica au la.
Bi Mwaniki alipinga hao wawili wakiachiliwa kwa dhamana akisema wako na uwezo wa kuwatisha na kuwavuruga mashahidi wasifike mahakamani kutoa ushahidi dhidi yao.
Kiongozi huyo wa mashtaka aliambia mahakama kuwa familia ya marehemu inapinga Bw Irungu akiachiliwa kwa dhamana ikitiliwa maanani jinsi Monica alivyouawa.
Jaji Wakiaga aliambiwa kuwa familia ya marehemu inaishi kwa hofu kwa vile “ inaona kama mauaji yake Monica ni njama za kuangamiza familia yao.”
Jaji Wakiaga alikataa ombi la vuguvugu la kuwatetea wanahabari likishiriki katika kesi hiyo .
Irungu na Maribe wamekanusha walimuua Monica mnamo Septemba 16, 2018. Waliofika mahakamani kuwapa washtakiwa moyo ni pamoja na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, aliyekuwa mkurugenzi wa masuala ya mawasiliano Ikulu Dennis Itumbi na mwanahabari kutoka kituo cha Televisheni cha Citizen Francis Gachuri.