Habari Mseto

Royal Media yakana kumtelekeza Maribe, yaomba apewe dhamana

October 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

SHIRIKA la Habari la Royal Media Services (RMS) ambalo ni mwaajiri wa mwanahabari wa runinga ya Citizen, Jacky Maribe, limejitokeza Alhamisi kukanusha kwamba limemtelekeza na kuiomba mahakama imwaachilie kwa dhamana likiahidi kuhakikisha hatoroki na anahudhuria vikao vya kesi kulingana na maagizo ya korti.

Bi Maribe na mchumba wake Joseph Irungu wanakabiliwa na mashtaka mazito ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani katika makazi yake mtaani Kilimani Septemba 19, 2018 ingawa wamekanusha mashtaka hayo mahakamani.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Mkurugenzi Mkuu wa RMS Wachira Waruru amesema kwamba mwanahabari huyo amekuwa na rekodi ya kupigiwa mfano kazini na hilo linawapa imani ya kuirai mahakama kumwaachilia kwa dhamana.

“Tunataka kuthibitisha kwamba Jacqueline Wanjiru Maribe ni mwajiriwa wa shirika la habari la Royal Media Services na alichukua livu ili kushughulikia masuala yake ya kibinafsi. Bi Maribe amekuwa na rekodi nzuri kazini na hajawahi kukabiliwa na ukosefu wa nidhamu,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo.

Shirika hilo vile vile limesema kwamba kwa muda wa miaka sita waliyotangamana na Bi Maribe, wanafahamu fika wa tabia na mienendo yake ndiposa wamejitokeza kuomba dhamana hiyo.

“Baada ya kupandishwa cheo kutoka ripota hadi mtangazaji wa habari kila ijumaa jioni, Bi Maribe alitwikwa mazitio ya kitaifa na kimataifa na aliyawajibikia vilivyo na kwa njia ya kuridhisha,” ikaongeza taarifa hiyo kama njia ya kukoleza dai lao la kutaka Bi Maribe awachiliwe.

Bi Maribe na Bw Jowi watajua hatima yao Jummnne Oktoba 30, 2018 wakati jaji  atatoa uamuzi kuhusu ombi lao la kuachiliwa kwa dhamana.