SGR yaleta vilio kwa maelfu ya Wakenya
NA ALLAN OLINGO
RELI ya kisasa ya SGR imegeuka kuwa kero kwa maelfu ya watu waliotegemea uchukuzi wa mizigo kwa matrela kujikimu kimaisha, miezi mitano pekee baada ya kuzinduliwa.
Maelfu ya watu wamefutwa kazi baada ya kampuni za malori zilizowaajiri kufungwa ama kupunguza shughuli zao.
Kampuni nyingi za mabohari ya mizigo (CFS) mjini Mombasa nazo zimefuta watu wengi kutokana na kupungua kwa kazi ama kuhamishia shughuli zao Nairobi.
Wafanyibiashara katika miji ambayo ilikuwa ikitegemea madereva wa malori pia wanaumia kutokana na athari za reli mpya. Miji hii ni pamoja na Mlolongo, Salama, Sultan Hamud na Mtito Andei.
Mambo yalianza kuwaharibikia wenye kampuni za malori, wafanyikazi wao na wafanyabiashara katika barabara ya Mombasa – Nairobi pale Shirika la Reli la Kenya (KR) mnamo Mei 30 lilipoanza uchukuzi wa mizigo kwa treni kutoka Bandari ya Mombasa hadi Kituo cha Kontena cha Nairobi (ICD).
Hatua hii ilipunguza idadi ya wateja waliosafirisha mizigo kwa matrela kwani walionelea afadhali kutumia treni kutokana na kasi yake pamoja na usalama wa mizigo yao. Hali hii iliathiri moja kwa moja kampuni za CFS. Kupungukiwa huku kwa biashara kulifanya nyingi ya kampuni za malori na CFS kupunguza idadi ya wafanyakazi.
Mapema mwezi huu, kampuni ya uchukuzi ya Bollore Logistics, ambayo ni moja ya zile kubwa za uchukuzi wa mizigo kanda ya Afrika Mashariki iliwafuta wafanyikazi wengi.
“Tutafanya mabadiliko ili tuwe na wafanyikazi wachache. Ni masikitiko kwani itatubidi tuwafute baadhi ya wafanyikazi,” Mkurugenzi Mkuu wa Bollore Kenya, Jean-Pascal Naud aliambia The East African.
Kulingana na Shirika la wenye CFS (CFSA), kufikia mwisho mwa mwezi Juni mwaka huu, watu 3,200 walikuwa wamefutwa kazi na kampuni hizo kutokana na kupungua kwa biashara.
“Ilibidi tufute nusu ya wafanyikazi. Hawa walikuwa wanafanya kazi hapa Bandari ya Mombasa kutokana na kupungua kwa kontena za kusafirishwa bara,” asema Daniel Nzeki, Afisa Mkuu wa CFSA.
Waziri wa Uchukuzi, James Macharia, naye asema kwamba zaidi ya madereva 1,300 wamepoteza kazi huku idadi hii ikitarajiwa kuongezeka kutokana na mipango ya Shirika la Reli kuongeza kiasi cha kontena zinazosafirishwa kwa treni hadi 250,000 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Inakisiwa kuwa kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka huu, wenye matrela watakuwa wamepata hasara ya Sh21 bilioni huku wenye CFS wakipoteza Sh10 bilioni. Hasara hii inatarajiwa kuwa kubwa zaidi kwani pia itaathiri kampuni za kuuza malori, vipuri, mekanika, wauzaji dizeli kwenye barabara ya Mombasa – Nairobi, wauzaji vyakula na vinywaji kwenye barabara hiyo na pia wenye vyumba vya malazi.
Mji wa Mombasa pia umeathirika pakubwa kutokana na upungufu wa matumizi ya pesa baada ya watu wengi kufutwa, wengine kurejea mashambani na umaskini kuongezeka.
Masaibu ya hasara ambayo imetokana na SGR yanajitokeza kwenye mahojiano na waathiriwa. Steve Kitili aliye na miaka 34 alikuwa ameajiriwa na kampuni moja ya CFS na alikuwa amepanda ngazi hadi cheo cha meneja. Lakini alipoteza kazi Juni mwaka huu baada ya mwenye kampuni kuhamia Nairobi.
“Sasa inanibidi nitegemee mke wangu kifedha. Hili si jambo rahisi,” aeleza Bw Kitili. Naye Bw Omar Bakari aliye na miaka 56, anasimulia kuhusu biashara ilivyobadilika tangu ujio wa SGR. Tulipatana naye alipokuwa akijiandaa kusafirisha Mitumba hadi mjini Kampala, Uganda: “Hii ni safari yangu ya kwanza mwezi huu lakini nashukuru. Kabla ya SGR, nilikuwa nikifanya safari tatu kwa mwezi na kupumzika wiki moja. Lakini sasa tunatumia muda mwingi tukisubiri mizigo kuliko tunavyotumia tukiwa barabarani. Mambo ni mabaya.”
Ishara ya mabadiliko yaliyoletwa na SGR kwenye biashara ya uchukuzi wa mizigo ni malori machache unayoona unapoendesha gari kwenye barabara ya Mombasa – Nairob. Hii ni kinyume na awali ambapo kwa kawaida matrela yalisababisha misongamano kwenye barabara hiyo.