Taharuki wanafunzi kutumiwa kadi ya rambirambi wakisubiri KCPE
JADSON GICHANA Na TITUS OMINDE
WALIMU na wanafunzi wa shule moja ya msingi katika Kaunti ya Kisii, walipatwa na mshangao jana walipopata kadi ya risala za rambirambi badala ya heri njema.
Kadi hiyo ilikuwa imetumwa kwa jina la diwani wa wadi ya Ichuni, Bw Gekonge Mirieri kwa watahiniwa wa KCPE wa shule ya msingi ya Bogeche.
“Pole kwa msiba mliopata. Tafadhali kubalini rambirambi zangu na familia yangu wakati huu mgumu,” kadi hiyo ilikuwa imeandikwa.
Wazazi walikashifu Bw Gekonge kwa kuwatumia watoto wao kadi kama hiyo ya rambirambi badala ya kadi ya heri.
Mwalimu mmoja alisema kadi hiyo ililetwa shuleni humo na mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Akiongea na Taifa Leo baadaye, diwani huyo aliwashtumu wapinzani wake kisiasa kwa kile alichosema ni kubadilisha kadi ya heri na kutuma ya rambirambi.
Alisema atawashtaki wale wote waliohusika kwa kumharibia jina.
Kwingineko, mwanafunzi wa kidato cha tatu alifikishwa katika mahakama mjini Eldoret jana kujibu mashtaka ya kujifanya mtahiniwa wa kike katika mtihani nadharia wa KCSE.
Mvulana huyo wa miaka 17, ambaye ni mwanafunzi katika shule ya upili ya Eden Faith Academy, Lugari, kaunti ya Kakamega alikabiliwa na shtaka la kusaidia watahiniwa wa kike kufanya mtihani wa kitaifa.
Alishtakiwa kuwa mnamo Oktoba 24 katika shule ya upili ya wavulana ya St Luke Lumakanda alipatikana akisaidia wanafunzi wa kike kutoka shule ya upili ya wasichana ya Mukuyu kufanya mtihani wa muziki kinyume cha sheria za baraza la mitihani nchini.
Wakati wa kukamatwa kwake, kijana huyo alikuwa akichezea watahiniwa hao ala ya Litungu
Alikana mashtaka mbele ya hakimu mkuu Charles Obulutsa na akaachiliwa kwa kwa dhamana ya Sh100,000.