Habari Mseto

Biashara Kenya kuimarika zaidi kampuni za Finland zikisaka nafasi

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Waziri wa Masuala ya Uchumi kutoka Finland Milka Lintila amewasili nchini kwa lengo la kukuza mauzo kati ya taifa hilo na Kenya.

Akiandamana na wajumbe zaidi ya 50 atakuwa nchini kati ya Jumatano na Jumamosi.

Wajumbe hao wamewakilisha kampuni tofauti na mashirika ya utafiti katika sekta za kidijitali, kawi, uchumi, teknolojia, madini na uchimbaji wa madini, elimu na afya.

Ziara hiyo ni katika kukuza ushirikiano wa kibiashara kati ya Finland na Kenya.

Balozi wa Finland nchini Kenya Bw Erik Lundberg alisema “Tuna furaha kuwa wenyeji wa wajumbe wengi hivi wa kibiashara. Nafasi zilizoko barani Afrika zimeanza kutambuliwa sana katika ajenda ya kisiasa ya Finland,” alisema na kuongeza kuwa Kenya ni nguzo kubwa ya katika kufungua nafasi za ushirika zaidi Barani Afrika.

“Kukuza na kuuza sera ya maendeleo na biashra ni sehemu pia ya mbinu ya kukuza maendeleo ya Finland,” alisema.

Kampuni za Finland na Kenya zitafanya mkutano Alhamisi kujadili nafasi za kibiashara katika sekta za elimu, afya na kawi.